Leodegar Tenga; Rais wa TFF |
Na Boniface Wambura
SEKRETERAITI ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo la 2012.
Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Serikali imeiingilia kati sakata la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.
Katika taarifa yake kwa Waandishi wa Habari jana, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imeeleza kuwa katiba ya sasa ya TFF si halali. Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa kuipitisha katiba hiyo ameondolewa.
Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.
Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee.
Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili kufuatilia kinachotokea nchini.
Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya.