Kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelo akizungumza na Waandishi wa Habari mchana huu Msimbazi. Kulia ni Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga. |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA
Msaidizi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC, Jamhuri
Mussa Kihwelo amesema kwamba Yanga wana pointi zao tatu sawa na Azam, hivyo
hawana shaka ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
mwishoni mwa msimu.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa klabu ya Simba SC, Mtaa wa
Msimbazi, Dar es Salaam mchana wa leo, Jamhuri maarufu kama Julio alisema
kwamba kwa sasa wanazidiwa pointi sita na Yanga, lakini anaamini mwisho wa
msimu watatetea ubingwa wao tu.
“Tutawafunga
Yanga na kuchukua pointi tatu, tutawafunga Azam FC na kuchukua pointi tatu na
sisi tunajua Yanga na Azam watafungwa pia mechi nyingine na sisi tutashinda
zote na kupanda kileleni,”alisema Julio.
Kwa
sasa katika msimamo wa Ligi Kuu, Yanga wapo kileleni kwa pointi zao 32, wakifuatiwa
na Azam yenye pointi 30, wakati Simba SC ina pointi 26.
Jamhuri
alisema kwamba Simba inaendelea vizuri na maandalizi yake ya mchezo wa
keshokutwa dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wana
matumaini makubwa ya kushinda.
Beki
huyo wa zamani wa Simba SC, alisema anafahamu JKT Ruvu ni timu nzuri na ngumu,
lakini hawataweza kuizuia timu yao kubeba pointi tatu hiyo kesho.