Na Bin Zubeiry |
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana imesimamisha kampeni za uchaguzi wa shirikisho zilizopangwa kuanza leo, kuelekea uchaguzi huo Februari 24, mwaka huu.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Lyatto jana imesema kwamba, Kamati yake imechukua hatua hiyo kutokana na Mamlaka iliyonayo Kikatiba.
“1. Kamati ya Uchaguzi, kwa mamlaka iliyonayo, kupitia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 3(1), 6(1) (g) na (l), 10(5), 11(6) inayosomeka pamoja na Ibara ya 14(1) na (2) na pia Ibara ya 26(5) na (6), imesitisha zoezi la kampeni za uchaguzi wa TFF na TPL Board lililokuwa lianze kesho tarehe 13/02/2013 hadi hapo itakapowatangazia, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakidhi kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF,”imesema taarifa hiyo ya jana.
Aidha, Taarifa ya Lyatto imesema; “2. Tarehe za Uchaguzi Mkuu wa TFF na TPL Board zinabaki kama zilivyopangwa. 3. Taarifa hii inazingatia pia Ibara ya 2(4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF inayoagiza uongozi uliopo madarakani kuendelea na kutekeleza majukumu ya Shirikisho hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika,”.
Hatua ya Lyatto kusitisha zoezi la kampeni, inafuatia Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF juzi kumuengua Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), Jamal Emil Malinzi kugombea nafasi ya urais, kwa madai hana uzoefu.
Taarifa ya TFF juzi, imesema kwamba mgombea pekee aliyepitishwa katika nafasi ya Urais, inayoachwa wazi na Leodegar Chilla Tenga anayeng’atuka ni Athumani Jumanne Nyamlani.
Malinzi aliwekewa pingamizi awali, lakini akashinda mbele ya Kamati ya Uchaguzi na baadaye akakatiwa Rufaa ambako juzi Kamati ya Rufaa imemuengua.
Nyamlani pia aliwekewa pingamizi, akashinda na akakatiwa Rufaa lakini pia ameshinda, baada ya pingamizi alilowekewa kutupiliwa mbali.
Wengine walioenguliwa ni Michael Wambura aliyekuwa akiwania nafasi ya Makamu wa Rais na Ahmed Yahya aliyekuwa akiwania nafasi ya Uenyekiti wa Bodi ya Ligi.
KUENGULIWA KWA MALINZI:
Malinzi ameenguliwa kwa madai hana uzoefu kwa mujibu wa Katiba, lakini mgombea huyo alisimama na rais wa sasa, Tenga katika uchaguzi uliopita mwaka 2008, akashindwa.
Huwezi kuona ni wapi Malinzi alipoteza sifa ya uzoefu kutoka mwaka 2008 hadi sasa anaenguliwa, kwa kuwa kwa kipindi chote hicho amebaki kuwa mdau wa kawaida wa soka, hadi filimbi ya uchaguzi mpya ilipopulizwa naye akaibuka tena.
Safari hii, Malinzi alionekana kujipanga vema mapema, akianzia kugombea KRFA, ambako alishinda.
Kwa sababu hiyo, inaonekana dhahiri Kamati ya Rufaa haijamtendea haki Malinzi.
Mapema jana, kundi la wapenzi wa soka liliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari, katika hoteli ya Travertine Magomeni na kuporomsha shutuma nzito dhidi ya Kamati hiyo, ambazo kama zina ukweli ndani yake ni doa kwa Kamati hiyo iliyoundwa hivi karibuni, kwa sura ya kupanua wigo wa demokrasia ndani ya shirikisho hilo.
Wapenzi hao wamesema wanaipa TFF siku tatu, kurudisha jina la Malinzi, vinginevyo wataandamana, ikibidi kwenda Mahakamani kuzuia uchaguzi huo.
Wameenda mbali, wakimtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuingilia kati suala la kuenguliwa kwa Malinzi kwani limefanywa kwa chuki binafsi likiwa na lengo la kumbemba mpinzani wake, Nyamlani.
Wamedai kuna mgongano wa kimaslahi ndani ya Kamati ya Rufaa juu ya uamuzi iliyochukua, wakitolea mfano, mmoja wa wana Kamati hiyo, Mbunge, Murtaza Mangungu ni mtu wa karibnu sana wa Nyamlani na Mwenyekiti wa Kamati, Iddi Mtiginjola amewahi kufanya na Nyamlani katika Mahakama ya Temeke na pia ni marafiki.
Wamedai, kwa kuwa Nyamlani hivi sasa ni Makamu wa kwanza wa rais wa TFF, alihusika kwa kiasi kikubwa kuunda Kamati hiyo, akiweka swahiba zake kwa lengo la kumsafishia njia ya kuingia Ikulu ya soka.
Hapo hapo, kuna pingamizi lililotupwa dhidi ya Nyamlani, kwamba Hakimu haruhusiwi kuongoza taasisi ambayo inaweza kufikishwa Mahakamani. Hili limetupwa, lakini ukizama ndani katika dhana ya mgongano wa kimaslahi, unaona kuna hoja hapa.
Tuhuma zilizotolewa dhidi ya Kamati ya Rufaa na hatua zilizochukuliwa na Kamati ya Uchaguzi zinaleta taswira fulani, sijui ipi nawaacha nanyi wasomaji wangu mtafakari.
Kama kweli Nyamlani aliwahi kufanya kazi na Mtiginjolo, rekodi zao zipo na zitasema kweli, iwapo zitahitajika katika kusaka ukweli wa tuhuma. Achana na hayo, kuenguliwa kwa Malinzi kumegubikwa na ukungu wa kile tulichozoea kusikia katika soka yetu; Fitina.
KWELI MALINZI SI MZOEFU?
Sababu inayotajwa kumuengua Malinzi katika kinyang’anyiro ni kukosa uzoefu, kwa mujibu wa Katiba anatakiwa awe ana uzoefu wa kuongoza sekta za michezo kwa miaka mitano.
Uzoefu wa aina ipi, lazima ifike wakati sifa hii ifafanuliwe na wadau waielewe vyema. Wakati Crescentius John Magori anagombea Umakamu wa kwanza wa Rais wa TFF miaka 10 iliyopita, uzoefu wake ulikuwa ni kutengeneza tovuti ya Simba na kuwa Makamu Mwenyekiti wa kundi la Friends of Simba kwa miaka isiyozidi miwili.
Damas Ndumdaro aligombea Umakamu wa Rais wa TFF katika uchaguzi uliopita mwaka 2008, sifa zake za uzoefu zikiwa ni kuwa ndani ya Kamati za kuteuliwa za TFF.
Unaweza kujionea mkanganyiko hapa- kanuni hii ya uzoefu haijakaa sawa, lazima ifafanuliwe.
Lakini pamoja na yote, hadi leo, Jamal Malinzi ana uzoefu wa miaka isiyopungua 12 katika uongozi wa soka nchini.
Mwaka 2000, Malinzi aliteuliwa kwa mara ya kwanza kwenye Bodi ya Seneti ya Yanga, wakati huo rais wa Yanga akiwa Tarimba Abbas na Desemba 31, mwaka 2001 ukafanyika uchaguzi, akashinda kwa kura nyingi kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa klabu, pamoja na akina Dk Kwera Mwaluvinga, David Lwimbo (wote sasa marehemu), Ibrahim Didi, Francis Kifukwe na Meckline Kahigi, chini rais Tarimba na Makamu wake, Mbaraka Igangula.
Wakati huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga alikuwa Lucas Kisasa, baada ya uchaguzi klabu ikaajiri Katibu Mtendaji, Arthur Irenge ambaye baada ya miezi miwili akaachia ngazi na Malinzi akawa anakaimu Ukatibu Mkuu Yanga, kuanzia Machi mwaka 2002 hadi ulipoitishwa uchaguzi Agosti mwaka 2003 akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa klabu na wanachama.
Malinzi aliendelea kuwa Yanga, lakini kutokana na desturi ya migogoro kwenye klabu zetu na mfumo wa wakati huo, Katiba dhaifu zilizokuwa zikichezewa na yeyote, mgombea huyo aliamua kujiengua ili kulinda heshima yake Mei 5, mwaka 2005.
Baada ya hapo, Malinzi aliendelea kuwa Mdau mkubwa wa mchezo wa soka, akihusishwa kwenye Kamati mbalimbali, ikiwemo ya timu ya mkoa wa Dar es Salaam, Mzizima alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi na akaiwezesha timu kutwaa Kombe mwaka 2007.
Pamoja na hayo, mwaka 2008 hadi mwaka 2010, Malinzi amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Chama cha Soka Pwani (COREFA),
2009 hadi 2102, amekuwa Mjumbe wa Baraza la Michezo Dar es Salaam, tangu mwaka 2011 amekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Kagera na tangu Machi mwaka 2012, amekuwa Mwenyekiti wa KRFA.
Tulikuwa na Malinzi Dakar, Senegal mwaka 2007 wakati Taifa Stars imekwenda kucheza na wenyeji na nakumbuka nchi nyingine pia ambazo Stars ilikwenda tuligongana naye mara kadhaa. Huyu ni mdau wa michezo na hakuna shaka juu ya hilo.
Na si yeye tu kama Jamal, ukoo wa Malinzi wote ni watu wa mpira, kaka yake Dioniz ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni Simba damu na amekuwa akisaidia mamilioni kuijenga klabu hiyo. Wamekuwa wakisaidia maendeleo ya soka Kagera hata kabla Jamal hajawa Mwenyekiti KRFA.
Kupitia kampuni yao, Cargo Stars wamekuwa wakisaidia michezo hususan soka. Huu ni ukoo wenye mapenzi na soka na haujutii hata waajiri wake kama Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kupoteza muda mwingi kwa ajili ya kufanya shughuli za soka.
HATIMA YA UCHAGUZI TFF
Kwa vurugu hizo zilizotokea hivi sasa, kuna wasiwasi mkubwa wa uchaguzi wa TFF kufanyika kama ulivyopangwa. Wapenzi wa Malinzi wanaweza kweli kwenda kuzuia uchaguzi Mahakamani, kwani uzoefu wa masuala kama haya unaleta wasiwasi huo.
Mwaka 2008 katika mashindano ya Kombe la Taifa, Tabora ilienguliwa kwa kumtumia mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’- lakini ukweli wa sakata lenyewe mkoa huo ulionewa. Kwa kutambua sheria haziruhusu mambo ya michezo kupelekwa mahakamani, TAREFA hawakwenda kortini, bali wapenzi wa soka wa mkoa ndio waliokwenda kuzuia mashindano hayo mahakamani.
Baadaye Tabora wakarudishwa kwenye mashindano na kesi ikafutwa, mashindano yakaendelea.
Wanaotaka kwenda mahakamani ni wakereketwa wa Malinzi, hao wapo tu siku nyingi hadi kwenye siasa na hawana hasara yoyote, kwa sababu nchi ikifutwa uanachama FIFA wao hawajali.
Hakika soka yetu imegota njia panda tena, tu kwa sababu ya fitina za uchaguzi, kuweka mbele maslahi binafsi baada ya mchezo wenyewe. Ni Wapi tunakwenda?