Wachezaji wa Azam |
REFA Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, ndiye atakayechezesha
mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na SC na
Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hashim atasaidiwa na Hamisi Chang’walu wa Dar es Salaam pia na
John Kanyenye kutoka Mbeya, wakati mezani atakuwepo Oden Mbaga.
Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi tatu, lakini macho na masikio ya
washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uwanja huo wa kisasa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga
na makamu bingwa Azam. Ingawa Azam imecheza mechi moja zaidi, lakini timu hizo
zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa
ligi huku kila moja ikiwa na pointi 36.
Pia vinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa wanatoka katika
timu hizo mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao tisa hadi sasa ndiye
anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao manane.
Iwapo timu yoyote itafanikiwa kuondoka na pointi tatu katika
mechi hiyo itakuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Hadi sasa, Yanga inaongoa ligi hiyo kwa pointi zake 36 sawa
na Azam, lakini ina mchezo mmoja mkononi na wastani mzuri wa mabao ya kufunga
na kufungwa.
Mechi nyingine za kesho ni Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu
itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Tanzania Prisons watakuwa
wenyeji wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jumapili (Februari 24 mwaka huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
utakuwa katika hekaheka nyingine kwa Simba chini ya Mfaransa Patrick Liewig
kuikabili Mtibwa Sugar inayonolewa na Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky
Maxime.