Mwenyekiti wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe. Leo watapata dinner na vijana Sapphire Court |
Na Mahmoud Zubeiry
VIGOGO wa kundi la Friends Of Simba, leo wanatarajiwa kupata chakula cha jioni na wachezaji wa Simba SC ikiwa ni siku mbili kabla ya timu hiyo kucheza mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola Jumapili.
Mwenyekiti wa F.O.S., Kapateni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba watawatembelea wachezaji wa timu hiyo katika kambi yao, hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam kupata nao chakula cha jioni.
“Tutazungumza nao ili kujua zaidi kuhusu wao na kuwapa hamasa ya kucheza kwa bidii, ili tuendeleze desturi ya Simba kufanya vizuri katika michuano ya Afrika,”alisema Hans Poppe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC.
Hans Poppe aliupongeza uongozi wa Simba, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage kwa kufanya kazi nzuri ya maandalizi ya timu kuanzia kambi ya Arusha na hadi sasa Dar es Salaam na kwamba ana matumaini Waangola watachapwa Jumapili.
“Tunajua hii timu ya Angola ni tajiri tajiri na imekuja hapa kwa kishindo na jeuri, ila jeuri yao tutaimaliza uwanjani Jumapili, Simba daima nguvu moja,”alisema Hans Poppe.
Kabla ya kuanza kwa michuano hii ya Afrika, Simba SC ilipata maandalizi ya kutosha, ikiwemo kushiriki Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na baadaye kwenda Oman kuweka kambi ya wiki mbili.
Iliporejea imefikia kwenye Ligi Kuu na kuanza na mechi ngumu tupu, ambazo imeshinda moja na kutoka sare mbili na sasa Jumapili inahamishia mawindo yake kwenye michuano ya Afrika. Kila la heri Simba SC.