Chuji; Simba na Azam wasahau ubingwa |
KIUNGO wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ amesema kwamba sasa Azam FC na Simba wajipange vema kugombea nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani ubingwa sasa ni wa Jangwani tu.
Kauli ya Chuji, inafuatia ushindi wa mabao 4-0 jana kwa timu yake dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi, Chuji alisema kwamba ushindi wa jana umefungua misuli yao na sasa watahakikisha wanashinda kila mechi hadi ubingwa.
“Hakuna atakayenusurika kwetu, ubingwa msimu huu ni wetu tu. Azam na Simba vema wakagombea nafasi ya pili, ubingwa wauheshimu sana, ni mali ya watu wazima hapa Dar es Salaam Young Africans, watoto wa Jangwani,”alisema kwa mbwembwe zote Chuji.
Yanga SC jana ilijitanua kileleni mwa Ligi Kuu, kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya African Lyon.
Matokeo haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 36, baada ya kucheza mechi 16, ikiwazidi Azam FC pointi tatu katika nafasi ya pili na mabingwa watetezi, Simba SC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 28.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari wanaongoza kwa mabao 2-0, ambayo yote yalitiwa kimiani na Jerry Tegete.
Tegete ambaye aliuanza mchezo huo vibaya akikosa mabao mawili ya wazi mwanzoni, kiasi cha mashabiki kuanza kupiga kelele za kutaka atolewe, alirekebisha makosa yake na kuwainua vitini mara mbili mashabiki hao kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo.
Alifunga bao la kwanza dakika ya 21, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya winga Simon Msuva, wakati la pili alifunga ‘Kizungu’ kwa kisigino baada Hamisi Kiiza kushindwa kuiunganisha krosi ya Juma Abdul na mpira ukampita na kumkuta mfungaji.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto zaidi, na kufanikiwa kuongeza mabao mawili, huku wakipoteza nafasi ya wazi ya kufunga bao moja zaidi kwa kupoteza penalti.
Hamisi Kiiza hakuwa mwenye bahati jana, kwani alikosa penalti dakika ya 47 baada ya kipa Abdul Seif kudaka, kufuatia beki Ibrahim Job kumchezea rafu Haruna Niyonzima kwenye eneo la hatari.
Didier Kavumbangu aliyeingia kuchukua nafasi ya Jery Tegete aliifungia Yanga bao la tatu kwa penalti dakika ya 69, baada ya beki Sunday Bakari kuunawa mpira kwenye mpira eneo la hatari.
Yanga ilihitimisha karamu yake mabao jioni ya jana kupitia kwa kiungo Nizar Khalfan aliyeingia kipindi cha pili pia kuchukua nafasi ya Simon Msuva, aliyefunga bao la nne dakika ya 80 kwa shuti akiunganisha krosi ya Saidi Bahanuzi, aliyetokea benchi pia kumpokea Kiiza.
Yussuf Mlipli alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90, baada ya kumchezea rafu David Luhende.
Refa Martin Saanya wa Morogoro alikimbizwa na wachezaji wa Lyon dakika ya 47 baada ya kuwapa penalti Yanga, na pamoja na wachezaji wengine kuonekana kumsukuma huku akikimbia hadi nje ya Uwanja, lakini alitoa kadi mbili tu na njano kwa Sunday Bakari na Yussuf Mlipili.
Wachezaji hao walitulizwa na kocha wa Salim Bausi, ambaye aliingia uwanjani baada ya kuona wanazidi kumtia kashikashi refa.
Refa msaidizi namba moja, Omar Kambangwa wa Dar es Salaam, alilazimika kuwaomba radhi wachezaji wa Yanga dakika ya 38 baada ya kumnyooshea kibendera cha kuotea Kiiza akiwa anakwenda kufunga, wakati beki mmoja wa Lyon alikuwa kwenye eneo la lango lao.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar, Frank Domayo, Jery Tegete/Kavu, Hamisi Kiiza/Bahanuzi na Haruna Niyonzima.
African Lyon; Abdul Seif, Yussuf Mlipili, Sunday Bakari, Ibrahim Job, Obina Salamusasa, Abdulghan Gulam, Amani Kyata, Mohamed Samatta, Iddi Mbaga/Mgwao/Jacob masawe, Bright Ike na Adam Kingwande/Benedict Mwamlangala.
Katika mechi nyingine, mabao ya Mohamed Jingo kwa penalti dakika ya 52 na James Magafu dakika ya 61 yaliipa Toto African sare ya 2-2 na Polisi Moro mabao yake yakifungwa na Kenneth Masumbuko dakika ya 57 na Nicholas Kabipe dakika ya 67 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Mtibwa Sugar nayo imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Mgambo JKT iliifunga JKT Oljoro mabao 2-0, mabao yake yakifungwa na Nassor Gumbo dakika ya sita na 43 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wenyeji Kagera Sugar waliifunga Coastal Union 1-0, bao pekee la Themi Felix dakika ya 65.