Brandts |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mholanzi, Ernie Brandts leo anatarajiwa kuiongoza Yanga katika mechi ya 18 ikimenyana na African Lyon ya Dar es Salaam katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, tangu ajiunge nayo Septemba mwaka jana, akitokea APR ya Rwanda.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, katika mechi 17 zilizopita, amepoteza tatu, moja ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba, na nyingine mbili katika mechi za kirafiki kwenye ziara ya Uturuki.
Mbali na kufungwa 1-0 na Kagera, chini ya Brandts Yanga ilifungwa 2-0 na Emmen FC ya Uturuki na 2-1 dhidi ya Denizlispor ya Uholanzi. Zaidi ya hapo, Brandts ametoa sare tatu, mbili katika Ligi Kuu dhidi ya Simba SC na Mtibwa Sugar, zote 1-1 na nyingine 1-1 pia katika mchezo wa kirafiki kwenye ziara ya Uturuki dhidi Ariminia Bielefed ya Ujerumani.
Katika mchezo wa leo, Yanga itahitaji ushindi ili kupaa kileleni mwa Ligi Kuu, kwani kwa sasa inalingana kwa pointi na Azam FC, 33 kila moja. Ushindi wa mabao 4-1 wa Azam dhidi ya Mtibwa Sugar mwishoni mwa wiki, umezidi kuisogeza Azam nyuma kabisa ya Yanga na sasa wana Jangwani hao wanaongoza kwa wastani wa mabao tu.
Yanga pia itahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya mashabiki wake, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa katika mchezo uiliopita.
Hadi sasa, ubingwa wa Ligi Kuu unaweza kuwa na sura ya farasi wa tatu, akiwemo Simba- lakini wawili wana hatua pana zaidi Yanga na Azam FC.
Mchezo unaonekana kubadilika kidogo tu kutoka msimu uliopita, wakati Azam na Simba zilipokuwa zinafukuzana kileleni, na sasa Yanga na Wana Lamba Lamba.
REKODI YA ERNIE BRANDTS YANGA
1. Yanga 1-1 Simba SC (Ligi Kuu)
2. Yanga 0-1 Kagera Sugar (Ligi Kuu)
3. Yanga 3-1 Toto African (Ligi Kuu)
4. Yanga 3-2 Ruvu Shooting (Ligi Kuu)
5. Yanga 3-0 Polisi Moro (Ligi Kuu)
6. Yanga 1-0 JKT Oljoro (Ligi Kuu)
7. Yanga 3-0 JKT Mgambo (Ligi Kuu)
8. Yanga 2-0 Azam FC (Ligi Kuu)
9. Yanga 2-0 Coastal (Ligi Kuu)
10. Yanga 0-1 Tusker (Kirafiki)
11. Yanga 1-1 Ariminia Bielefed (Kirafiki)
12. Yanga SC 0-2 Emmen FC (Kirafiki)
13. Yanga SC 1-2 Denizlispor FC (Kirafiki)
14. Yanga SC 3-2 Black Leopard (Kirafiki)
15. Yanga SC 2-1 Black Leopard (Kirafiki)
16. Yanga SC 3-1 Prisons (Ligi Kuu)
17. Yanga 1-1 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
18. Yanga SC Vs Africans Lyon (Ligi Kuu)