Haruna Moshi 'Boban' akipinduka na mtu kwenye penati box. Sasa amani anatia timu Arusha |
Na Mahmoud Zubeiry
KIKAO cha pamoja baina ya uongozi wa Simba SC na wachezaji wao wawili tegemeo, Mrisho Khalfan Ngassa na Haruna Moshi Shaaban leo mchana kimekuwa chenye mafanikio na wachezaji hao wataondoka kesho Dar es Salaam kwenda Arusha kuungana na timu tayari kwa mchezo dhidi ya wenyeji JKT Oljoro Jumamosi.
Kikao hicho kilifanyika, kufuatia kesi iliyowasilishwa dhidi ya nyota hao kwa uongozi na Kocha Mfaransa, Patrick Liewig.
Habari za uhakika, kutoka ndani ya Simba SC, zimesema kwamba, pande zote zimekubaliana kusonga mbele kwa manufaa ya Simba. "Lengo hapa ni kuijenga Simba SC, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi, kwa hiyo tumefikia mwafaka na wachezaji kesho wanaenda Arusha,"kilisema chanzo kutoka Simba SC.
Kikosi cha Simba SC kimeondoka leo asubuhi kwenda Arusha tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, lakini Haruna maarufu kama Boban na Ngassa walibaki kwa ajili ya kikao hicho.
Kumekuwa na habari za kizushi sana eti, wachezaji hao wamesimamishwa kwa utovu wa nidhamu, lakini ukweli ni kwamba hawajasimamishwa na wala uongozi hauna dhamira ya kufanya hivyo kwa kuwa hawana kosa kubwa, zaidi ya kutofautiana na kocha.
BIN ZUBEIRY inafahamu Simba haiko tayari kuvuruga timu yake kwa sasa zaidi ya kujipanga sawasawa, ili kuhakikisha wanajiimarisha kwenye mbio za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na pia kupigiania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.