Bin Kleb |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema
kwamba wanaihofia sana Azam FC kuliko Simba SC katika mbio za ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Kleb alisema kwamba hadi sasa safari bado ni ndefu
kuelekea kwenye kilele cha ubingwa na timu zote tatu, Yanga, Azam na Simba SC
zina nafasi ya kutwaa taji hilo.
“Lakini
kwa mwenendo wa ligi jinsi ulivyo, kuna kila sababu ya kuihofia Azam kuliko Simba
ambao ni mabingwa watetezi. Kwanza hawa ndio wapo nyuma yetu tukiwa tunawazidi
pointi tatu tu. Pili, ni timu nzuri na ina nyenzo za kutosha za kupambana,”alisema
Bin Kleb.
Mwenyekiti
huyo alisema anafurahia ushindani uliopo katika Ligi Kuu, kwani ni kipimo
kizuri kwa timu na ndiyo maana wao wameamua kujipanga upya kwa ajili ya mechi
zijazo.
“Tumetoa
sare ambayo kwa kweli haikutarajiwa (dhidi ya Mtibwa), tumepunguza idadi ya
pointi ambazo tulikuwa tunawazidi Azam kutoka tano hadi tatu, sasa hii maana
yake tukiteleza tena, watatukamata, hatuko tayari kwa hilo, tunajipanga upya
kuelekea mechi zijazo,”alisema Bin Kleb.
Bin
Kleb alisema kwamba wana imani na timu yao na maandalizi waliyofanya kabla ya
kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hivyo ndoto za ubingwa zipo pale pale. “Matumaini
ya ubingwa yapo sana tu, nachozungumzia hapa ni changamoto ambazo tutakabiliana
nazo, ndiyo kama hivyo Azam ni timu ambayo tunaihofia zaidi kuliko Simba,”alisema.
Yanga
ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 33, ikifuatiwa na Azam yenye 30,
wakati SImba ina pointi 27, timu zote zikiwa zimecheza mechi 15 kila moja.