Bin Kleb kulia akizungumza na Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema kwamba
hakuna suala la ushirikina ndani ya klabu yao, bali kuna watu ambao ni
wapinzani wao wanapandikiza chuki kwa wachezaji wao, ili kuvuruga umoja na amani
iliyopo ndani ya kikosi chao kwa sasa.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Bin Kleb alisema kwamba amesikia wapo wachezaji walitaka
kushikana mashati mazoezini wakituhumiana kulogana, lakini baada ya uongozi
kulifanyia kazi suala hilo, umegundua kuna watu wanapandikiza chuki baina ya
wachezaji wao hao.
Mshambuliaji
Mrundi, Didier Kavumbangu anadaiwa kumvaa Jerry Tegete na kumtuhumu kwamba
anamloga kumpunguza kasi uwanjani, ili ang’are yeye.
“Hakuna
kitu kama hicho, kuna watu wanawachonganisha hawa wachezaji, wewe fikiria sasa
wao ndio wanacheza kama washambuliaji pacha na wanaelewana sana, hakuna
anayekaa benchi kati yao, sasa hilo suala la kulogana linatoka wapi?”alihoji
Bin Kleb.
Kiongozi
huyo alisema jambo ambalo anaweza kukiri ndani ya Yanga hivi sasa ni ushindani mkubwa wa namba ndani ya kikosi
kizima na ili mchezaji apate nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lazima afanye
kazi haswa.
“Tumezungumza
nao wachezaji na tutaendelea kuzungumza nao, wanapaswa kuwa makini, mtu kama
hafanyi vizuri atafute sababu za msingi za kitaalamu na si kutuletea mambo ya Kiswahili
kwenye timu.
Leo
ukipandikiza chuki eti Tegete anamloga Kavumbangu, kwa sababu Tegete anafunga
na Kavumbangu hafungi, je wakati wa mzunguko wa kwanza Kavumbangu alipokuwa anafunga
Tegete hafungi, nani alikuwa anamloga mwenzake?”alihoji Bin Kleb.
Kiongozi
huyo amesema kwamba wanapocheza washambuliaji wawili kama pacha lazima mmoja
ndiye awe anafunga sana na wengine watafunga zikitokea nafasi. “Angalia hata
Manchester United, Wayne Rooney ndiye alikuwa mfungaji wa timu, lakini kasajiliwa
Van Persie mambo yamebadilika. Van Persie ndiye anafunga sana sasa hivi,
ikitokea Rooney akapata nafasi naye anafunga. Huwezi kusikia mtu Analia kalogwa,”alisema
Bin Kleb.
Kleb
amewaasa wachezaji wa Yanga kuwa makini na watu wenye lengo la kuwachonganisha
kuvuruga amani iliyopo ndani ya kikosi chao kwa sasa ambayo ndiyo siri ya
mafanikio yao, ikiwemo kutwaa Kombe la Kagame, kuongoza Ligi na kwa ujumla
kufanya vizuri.
“Tunaelekea
kuzuri, sasa vema wachezaji wetu wakatuliza sana akili zao na kuwa makini na
adui zetu, wanaotaka kuwavuruga ili timu ishuke kiwango,”alisema.
Yanga
inatarajiwa kushuka dimbani tena leo kucheza mechi ya pili ya mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, mchezo
ambao utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo wake wa kwanza, Yanga ilishinda 3-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya na kuzidi
kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 32, ikifuatiwa na
Azam yenye pointi 30 na Simba pointi 26. Ikumbukwe, katika mechi yha mzunguko
wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro.