RAFA Benitez anaifikiria kazi ya Jose Mourinho katika klabu ya Real Madrid wakati huu ambao anajipanga kuachana na Chelsea mwisho wa msimu huu.
Benitez anaamini mapenzi yake kwa Real Madrid yatambeba wakati klabu hiyo itakapo kuwa inatafuta mrithi wa Mourinho.
Mhispaniola huyo alisema: “Nilitua Real (Madrid) wakati nikiwa na miaka 13 na mimi nimetoka Jiji la Madrid.
“Kama kocha lazima utakuwa na kipenzi chako. Ninauhusiano na mashabiki na walipokea vizuri. Lakini sitaki kujihusisha na uvumi.
“Nina mkataba na Chelsea mpaka mwisho wa msimu na nitafanya kila niwezalo kuhakikisha naipa mafanikio klabu hii.” Alisema Benitez,
Benitez ambaye alianza kucheza soka lake kwenye klabu ya Real Madrid na baadaye kufanya kazi kama kocha wa vijana, pia anaitolea macho kazi ya Vicente del Bosque, katika timu ya taifa ya Hispania. Mkataba wa Del Bosque unafikia tamati 2014, na Benitez alisema kwamba anauhusiano mzuri na kocha huyo lakini hawezi kukanusha uwezekano kuifundisha timu hiyo siku Del Bosque akiondoka.
Ni Jambo nitaliangalia siku za usoni, Japokuwa natakiwa kuendelea kuwa mkufunzi wa soka.” Kocha huyo wa muda Chelsea amekiri kwamba itakuwa ngumu kwake kuwashawishi mashabiki wa klabu hiyo wampende. “Tatizo kubwa ni kwa sababu niliwahi kuwa kocha wa Liverpool,” alisema. “Na ninahukumiwa kwa mafanikio niliyoyapata nikiwa Liverpool.
“Pamoja na yote hayo, nitaendelea kufanya kazi kwa nguvu, nimejizatiti kupata mafanikio nikiwa na Chelsea.”
Wakati huo huo, Mbelgiji, Thibaut Courtois amesisitiza yeye ndiye mtu sahihi wa kuchukua nafasi ya Petr Cech, Stamford Bridge. Courtois, (20), alisajiliwa kutoka Genk mwaka 2011 lakini kwa sasa yuko kwa mkopo Atletico Madrid, alisema: “Wataendelea kuwa na Cech kwa miaka miwili ijayo. Chelsea hawakutegemea ningefikia kiwango hiki haraka hivi.”