Kipre Balou |
Na Mahmoud Zubeiry
WACHEZAJI wawili wa Azam FC, Kipre Michael Balou kutoka Ivory Coast na Brian Umony wa Uganda, walioumia katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shiriksiho Afrika dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, wanaendelea vizuri.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wawili hao hata kama hawataweza kucheza mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu, lakini Jumamosi watacheza dhidi ya Yanga.
Ongala amesema Balou jana alianza mazoezi ya gym, wakati Umony alishindwa kabisa kufanya mazoezi. “Ila Umony amenihakikishia mechi ya Yanga atacheza, amesema anaendelea vizuri, alipumzika jana lakini leo anaweza kuanza mazoezi,”alisema Ongala.
Aidha, kiungo Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ amekwenda kwao visiwani Zanzibar kushiriki msiba na hatakuwepo kesho timu hiyo ikimenyana na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Beki Waziri Salum anaendelea vizuri na anafanya mazoezi, akiwa kwenye nafasi nzuri ya kucheza kesho kwa mara ya kwanza tangu Desemba, mwaka jana alipoumia.
Ongala amesema timu ipo kambini tangu juzi Chamazi kujiandaa na mechi hizo mbili za Ligi Kuu kwa pamoja na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Nasir.
Azam ilianza vema kampeni zake za michuano ya Afrika, baada ya kuilaza Nasir mabao 3-1 na sasa inahitaji hata sare au kufungwa si kwa zaidi ya tofauti ya bao moja katika mchezo wa marudiano wiki ijayo Sudan Kusini ili kusonga mbele.