Kikosi cha Azam |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC iko tayari kuonyesha makali yake katika michuano ya Afrika wakati itakapoanza kupeperusha bendera ya Tanzania katika Kombe la Shirikisho kesho.
Azam inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kumenyana na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa klabu hiyo iliyoanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2008 kucheza michuano ya Afrika, baada ya msimu uliopita kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu, nyuma ya Simba SC, ikiwapiku vigogo Yanga.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Muingereza Kali Ongala ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba timu imekuwa kambini tangu Jumanne wiki hii katika hosteli zao zilizopo Chamazi, ndani ya Azam Complex kujiandaa na mchezo huo.
Kali amesema maandalizi yamekuwa mazuri na wachezaji wana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo. Amesema ni wachezaji wawili tu majeruhi, ambao ni mabeki Samih Hajji Nuhu na Salum Waziri, lakini wengine wote wapo fiti.
John Bocco ‘Adebayor’ ambaye amekuwa nje ya Uwanja tangu Desemba mwaka jana kwa matatizo ya goti, anaweza japo kuanzia benchi kwenye mechi ya kesho.
“Bocco yuko fiti kwa sasa, hata kama haifiki asilimia 100, lakini siyo chini ya 80, na anaweza japo kuanzia benchi kesho,”alisema Kali.
Azam jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kuzoea mandhari ya Uwanja huo kabla ya kipute hicho kesho. Na kwa kuwa Al Nasir watakuja kesho, Azam wanaangalia uwezekano wa leo pia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, ili wauzoee vyema zaidi.
Azam imepata maandalizi mazuri kabla ya michuano ya Afrika, ikianza kwa kushiriki michuano ya Kombe la Hisani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako walitwaa ubingwa Desemba mwaka jana, baadaye Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar walilotwaa pia.
Kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, Azam walikwenda kucheza mechi tatu za kirafiki Kenya, ambako walishinda mbili na kufungwa na moja katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, Azam wameshinda mechi zao zote tatu za mwanzoni- hii ni kuashiria kwamba kikosi kipo imara.
Kila la heri Azam FC.