Na Bin Zubeiry |
SHANGWE za Uturuki, Uturuki zilivuma kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, mashabiki wa timu yao wakisherehekea ushindi wa mabao 3-2 dhidi
ya Black Leopard ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki.
Yanga iliyokuwa kwenye kambi ya mafunzo nchini Uturuki kwa
wiki mbili kabla ya kurejea Dar es Salaam, katika mchezo wa jana, hadi
mapumziko, walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake
aliyefufua makali, Jerry John Tegete dakika ya 33.
Tegete, alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya
kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima kuangushwa kwenye
eneo la hatari na beki Nkosiyaba Xakane na refa Hashim Abdallah wa Dar es
Salaam akatoa adhabu hiyo.
Kipindi cha pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts
alifanya mabadiliko, akiwatoa pacha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) wenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa
‘Barthez’ na kuwaingiza Simon Msuva, Juma Abdul na kipa Said Mohamed.
Mabadiliko hayo, hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard
walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya kwanza tu tangu kuanza kipindi cha
pili, lililofungwa kwa kichwa na Humphrey Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa
timu hiyo ya Jangwani na kumtungua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa
kupata bao la pili dakika ya 63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi
maridadi ya Niyonzima.
Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha
pasi ya beki Juma Abdul na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe
za ‘Uturuki, Uturuki’, kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini
Uturuki kwa wiki mbili zilizopita.
Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la
hatari Humphrey Khoza dakika ya 88 na refa akawapa penalti Leopard ambayo
ilikwamishwa kimiani na Rodney Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.
Tena katika mchezo huo, Yanga ilipanga kikosi chake kamili,
langoni akianza Ally Mustafa ‘Barthez’ ambaye kipindi cha pili akampisha Said
Mohamed, kulia Mbuyu Twite aliyempisha Juma Abdul kipindi cha pili, kushoto Oscar
Joshua, katikati kama kawaida Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, kiungo
mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’, viungo wengine Kabange Twite aliyempisha Simon
Msuva, Frank Domayo na Haruna Niyonzima, wakati washambuliaji walikuwa ni Jerry
Tegete na Didier Kavumbangu aliyempisha Said Bahanuzi dakika ya 75.
Huu unaweza kusema ni ‘mziki’ wa Yanga kwa sasa, labda
kakosekana Hamisi Kiiza ambaye ni mgonjwa katika wachezaji ambao hupewa nafasi
kwenye kikosi cha kwanza.
Kwa kweli nilisikitika sana jana kuona mashabiki wa Yanga
wanashangilia mno ushindi huo wa 3-2 nyumbani, dhidi ya timu ambayo kwa kwa
namna yoyote huwezi kukwepa kuiita kibonde, kwa sababu haifanyi vizuri katika
Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Black Leopard yenye maskani yake Polokwane, Limpopo nchini Afrika
Kusini kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini na msimu
uliopita ilinusurika kushuka Daraja, ikishika nafasi ya 14 katika Ligi ya timu
16.
Leopards ilirejea Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka juzi tangu
ishuke 2008 na huwezi kuichukulia kama timu ya ushindani kulingana na matokeo
yake.
Yanga ilikuwa Uturuki kwa wiki mbili kwa kambi ya mazoezi na
ilirejea Jumapili iliyopita mjini Dar es Salaam. Katika ziara yake hiyo,
ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu na kufungwa mbili na kutoka sare moja.
Katika mchezo wake wa kwanza, ilitoka sare ya 1-1 Ariminia
Bielefeld ya Daraja la Tatu (sawa na la nne) Ujerumani kabla ya kufungwa 2-1 na
Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na baadaye 2-0 na Emmen FC ya Ligi
Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga iliweka kambi katika hoteli ya Fame Residence Lara
& Spa kilomita chache kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Jiji la Antalya, iliyopo
ufukweni mwa bahari ya Mediteranian.
Kikosi cha wachezaji 27 kilikuwa kambini nchini Uturuki,
ambacho ni makipa; Ally Mustafa 'Barthez', Said Mohamed na Yussuf Abdul, mabeki
Juma Abdul, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua,
Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladisalus Mbogo na Kelvin Yondani.
Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna
Niyonzima, Kabange Twite, Nurdin Bakari, Omega Seme, Simon Msuva, Rehani
Kibingu, Nizar Khalfani na David Luhende wakati washambuliaji ni Didier
Kavumbagu, Said Bahanunzi, Jerry Tegete, George Banda na Hamisi Kiiza na Kocha
Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro na Kocha wa
makipa na Razak Ssiwa.
Hiyo inakuwa mara ya tatu kihistoria Yanga kufanya ziara nje
ya Afrika baada ya Brazil mwaka 1975 na Romania mwaka 1978. Yanga pia imewahi
kuweka kambi Afrika Kusini mwaka 2008.
Soka ni mchezo wa makosa, hata kama Yanga walivutiwa kiwango
cha uchezaji wa timu, kwa maana ya kumiliki mpira, kuonana kwa pasi za uhakika
na kadhalika, lakini watathmini matokeo na aina ya timu waliyocheza nayo.
Hawawezi kukutana na timu ya aina hiyo katika Ligi ya
Mabingwa Afrika mwaka 2014, watakutana na timu madhubuti.
Lakini hata wakikutana na timu ya aina hiyo, kama nyumbani wameshinda
mabao 3-2, kweli mchezo wa ugenini wanaweza kunusurika? Maana yake sasa Leopard
wangekuwa wanahitaji ushindi wa 1-0 wafuzu. Ingekuwa hatari.
Mimi najua tatizo moja kubwa la watu wa Yanga na hata Simba,
wanapenda kusifiwa tu. Na hili limekuwa ndio desturi katika kipindi hiki cha
mfumuko wa magazeti ya kimichezo, yaliyokariri ‘Yanga inauza’, basi wanaandika
vichwa vya habari vya kuisifia mno Yanga, ili wauze magazeti, wakati ukienda
kwenye hali halisi ni mambo tofauti.
Hii nini maana yake, wanawajaza ujinga Yanga, mwakani
wanaingia Ligi ya Mabingwa hawafiki popote.
Tafakari, tangu Novemba mwaka jana Yanga imekuwa mazoezini,
baada ya hapo mwishoni mwa Desemba ikaenda Uturuki, kambi ya wiki mbili. Imefika
Dar es Salaam imepata wiki nzima ya kujiandaa na mchezo na Leopard, halafu inakwenda
kushinda 3-2.
Huwezi kuulaumu uongozi kwa lolote, umetekeleza wajibu wake
kuhakikisha timu inapata maandalizi ya kutosha, lakini timu sasa, kwa maana ya
benchi la ufundi na wachezaji ndio wanapaswa kuwajibika kwa matokeo haya.
Lazima viongozi wa Yanga waepuke kuwa mashabiki na wasimame
kama viongozi, ambao daima wataangalia mambo kitaalamu na kuzingatia dira
waliyojiwekea. Wakati fulani, mwanzoni mwa Ligi Kuu msimu huu mzunguko wa
kwanza, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Bin Kleb
aliwafokea wachezaji na kocha Ernie Brandts kwamba pamoja na timu kushinda 3-0
dhidi ya Mgambo JKT, lakini ilicheza soka mbovu.
Baada ya mkwara huo, nilishuhudia mabadiliko makubwa ya
kiuchezaji katika mechi zilizofuata za Yanga, wapinzani walikuwa wanausaka
mpira kwa tochi kweli. Azam alipigwa 2-0 na alizidiwa mno kisoka na hata
viongozi wake siku hiyo walikiri.
Najua Yanga wanapenda sifa za vichwa vya habari, lakini haziwasaidii,
zinawabomoa na umefika wakati sasa wajiulize ndani ya miaka karibu 80 ya kuwepo
kwao kama klabu wana nini cha kujivunia katika dunia ya soka?
Hapa nyumbani kwenyewe, shabiki wa Yanga akikutana na shabiki
wa Simba hana raha masikini, atakumbushwa 5-0 za msimu uliopita, atakumbushwa
na zile 6-0, basi atainamisha kichwa chini tu.
Makosa yaliyoruhusu Leopard kupata mabao mawili jana,
yanapaswa kupewa kipaumbele na benchi la ufundi la Yanga kuelekea mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu. Niliwahi kusema mapema, Yanga wana fursa nzuri ya kutengeneza
timu imara kabla ya kurudi kwenye michuano ya Afrika mwakani.
Lakini wasidanganye na kuongoza Ligi, Simba inajinoa Oman,
inapata mechi ngumu, inafungwa lakini inajifunza. Azam sasa hivi wapo Kenya
wanajinoa, wanapata mechi ngumu, jana wamefungwa, lakini wanajifunza. Dhahiri,
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu utakuwa mgumu, hivyo Yanga wasikubali sifa za
kijinga, watengeneze timu yao. Jumapili njema. Nawatakia kila la heri, katika Mkutano wao Mkuu leo.