Vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Tanzania Prisons ya Mbeya katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo. Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa pointi zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikiizidi mbili Azam iliyocheza mechi 14 na tatu Simba SC iliyocheza 14 pia, ikishinda leo itaongeza idadi ya pointi za kuwazidi wapinzani wake hao katika mbio za ubingwa kama ilivyokuwa baada ya mzunguko wa kwanza. Katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo baina ya timu hizo mjini Mbeya, Yanga ililalizimishwa sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Jeshi la Magereza. Mambo yatakuwaje leo Uwanja wa Taifa, ikikumbukwa Yanga iliweka kambi ya wiki Uturuki, kujiandaa na hatua hii ya salama? twendeni Taifa tukashuhudia jioni ya leo, Prisons ikiongozwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Emmanuel Gabriel Mwakyusa aliyekuwa mwiba kwa wana Jangwani hao, enzi zake akivaa jezi nyekundu ya Msimbazi.
|