Yanga SC |
Na Prince Akbar
YANGA SC
inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo kumenyana na Black
Leopard ya Afrika Kusini, huo ukiwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo
ndani ya siku nne.
Awalil, timu
hizo zilimenyana Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga ikashinda
mabao 3-2.
Huo utakuwa
mchezo wa mwisho wa kujipima nguvu kwa Yanga, kabla ya kuingia mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu hya Vodacom Tanzania Bara unaoanza mwishoni mwa wiki.
Mabingwa hao
wa Afrika Mashariki na Kati, katika kujiandaa na mzunguko huo wa pili wa Ligi
Kuu, waliweka kambi ya wiki mbili Jijini Antalya, Uturuki kuanzia Desemba 30
mwaka jana hadi Januari 12 mwaka huu.
Katika kambi
hiyo, pamoja na kufanya mazoezi ya nguvu ya ufukweni, uwanjani na gym, Yanga
ilipata mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya Ariminia Bielefed ya Daraja
la Nne Ujerumani waliyotoka nayo sare ya 1-1, kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya
Daraja la Kwanza Uturuki na 2-0 na Emmen FC ya Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga
ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi
zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi
zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23.
Katika
mchezo wa kwanza na Leopard Dar es Salaam, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele
kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wake aliyefufua makali, Jerry
John Tegete dakika ya 33.
Tegete,
alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo wa kimataifa wa
Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki
Nkosiyaba Xakane na refa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam akatoa adhabu hiyo.
Kipindi cha
pili, kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alifanya mabadiliko, akiwatoa
pacha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wenye uraia wa Rwanda,
Mbuyu Twite na Kabange Twite na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwaingiza Simon
Msuva, Juma Abdul na kipa Said Mohamed.
Mabadiliko
hayo, hayakuisaidia Yanga, kwani Leopard walifanikiwa kusawazisha bao hilo
dakika ya kwanza tu tangu kuanza kipindi cha pili, lililofungwa kwa kichwa na
Humphrey Khoza aliyetumia udhaifu wa mabeki wa timu hiyo ya Jangwani na
kumtungua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya
kufungwa bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya
63, lililofungwa na Frank Domayo aliyeunganisha krosi maridadi ya Niyonzima.
Jerry Tegete
aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72 akiunganisha pasi ya beki Juma Abdul
na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waruke kwa shangwe za ‘Uturuki, Uturuki’,
kuashiria hayo ni matunda ya ziara ya timu hiyo nchini Uturuki.
Beki Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ alimuangusha kwenye eneo la hatari Humphrey Khoza dakika ya
88 na refa akawapa penalti Leopard ambayo ilikwamishwa kimiani na Rodney
Romagalela na kufanya matokeo yawe 3-2.
Katika
mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa, Yanga; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu
Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi
‘Chuji’, Kabange Twite, Frank Domayo, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Haruna
Niyonzima.
Black
Leopard; Ayunda Mtshati, Ernort Zaga, Nkosiyaba Xakane, Harry Nyirenda,
Humphrey Khoza, Muganga Dyange Jean, Mongezi Bobe, Thomas Madiba, Abbas Amidu,
Edgar Manake na Rodney Romagalela.