Mfungaji wa mabao mawili ya Yanga jana, Jerry Tegete kushoto akiwatoka wachezaji wa Prisons |
Na Prince Akbar
KWELI Yanga ni mtambo wa kutengeneza fedha, acha wajanja
waitumie kujinufaisha. Wakati mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, kati ya Simba SC na African Lyon juzi iliingiza kiasi cha Milioni 53 tu,
mchezo wa jana wa ligi hiyo kati ya Yanga na Tanzania Prisons umeingiza Sh. Milioni
101.
Jumla ya kiasi kilichopatikana katika mchezo huo ambao ni Sh.
101,016,000 ikiwa ni karibu zaidi ya nusu ya pato la mchezo wa juzi.
Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Boniface Wambura imesema mechi hiyo namba 94 iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, watazamaji 17,946 walikata
tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh.
15,000 na sh. 20,000.
Wambura amesema watazamaji 16,158 kati ya hao walikata tiketi
za sh. 5,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ni 98 waliokata tiketi za
sh. 20,000 na kila klabu imepata mgawo wa sh. 24,314,752.45 wakati Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 15,409,220.34. Asilimia 15
iliyokwenda kwenye uwanja baada ya kuondoa VAT na gharama za tiketi ni sh.
12,363,433.45.
Amesema mgawo mwingine wa mapato hayo ni tiketi sh.
3,183,890, gharama za mechi sh. 7,413,060.07, Kamati ya Ligi sh. 7,418,060.07,
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,709,030.03 na Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,884,801.14.
Ikumbukwe mechi namba 92 juzi Uwanja wa Taifa pia iliyomalizika
kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya African Lyon, iliingiza Sh.
53,756,000.
Watazamaji 9,408 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo
iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000
huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 12,499,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya Uwanja sh.
6,355,806.33, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati
ya Ligi Sh. 3,813,483.80, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh.
1,906,741.90 na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,483,021.48.