WIKI
iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa,
Ridhiwani Kikwete, alizungumzia mifumo ya uendeshwaji wa klabu za Simba na Yanga
za Dar es Salaam.
Na Bin Zubeiry |
Kwa ujumla,
Ridhi hakuridhishwa na mifumo hiyo, lakini kwa kuilinganisha akasema afadhili
kidogo wa Simba SC, kwa sababu wao fedha za kujiendesha hutokana na michango ya
wadau wake, lakini wa Yanga ni mbovu zaidi, kwa sababu unategemea fedha kutoka
kwenye mfuko wa mtu mmoja.
Mtoto huyo
wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizungumza hayo wakati anatoa
hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) Jumamosi katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani
Pwani.
Katika mada
yangu iliyopita niliunga mkono hoja hiyo, isipokuwa nilizama ndani hadi
nikawakera baadhi ya swahiba zangu wa Yanga, ndiyo changamoto za kazi hizo.
Nilipokea
maoni ya wengi baada ya makala hiyo, wenye hekima na wasio na hekima, wenye
busara na wasio na busara, weledi na wasio weledi na kila mmoja aliwasilisha
kwa mtazamo wake. Niliyapokea yote. Wenye kunitukana ‘alhamdulillah’, wenye
kunipongeza ‘mashaallah’.
Kwa sasa
mimi ni mwandishi mkomavu, sijibizani na wasomaji, hasa wale wanaotaka
kupingana na mimi bila hoja, ila napitia mawazo yao ili kujua namna ya kuwasaidia
zaidi.
Nataka
niwaambia kitu kimoja Yanga, wamebahatika kuwa na viongozi wenye uwezo wa
kifedha, wasomi na kwa ujumla viongozi wa kisasa. Si Manji, tu hata Wajumbe
wengine karibu wote wa Kamati ya Utendaji ya Yanga si watu wenye ‘njaa’.
Hii maana
yake ni kwamba klabu yao ipo katika mikono salama chini ya viongozi hawa, na
ndiyo maana timu ipo Uturuki hivi sasa kwenye kambi ya mafunzo ya wiki mbili.
Lakini wana
Yanga wanatakiwa kujua, fedha za Mwenyekiti wao, Alhaj Yussuf Manji au za
Makamu, Clement Sanga na hata Mjumbe, Abdallah Bin Kleb, si fedha za Yanga.
Bali sasa,
wawahimize hawa Matajiri wao, waitengenezee klabu uwezo wa kujitegemea, ili
siku moja na wao waongoze klabu bila kutumia fedha zao na hata wakitumia, iwe
kwa utashi na si kulazimika kama ilivyo sasa.
Sina shaka
na viongozi wa Yanga katika suala la uwezo wa kifedha, lakini hakuna siri Yanga
pamoja na rasilimali zake ilizonazo, bado haina cha kujivunia.
Tayari Yanga
ina misingi ambayo inahitaji kuendelezwa kama majengo yake mawili, la Mtaa wa
Jangwani na la Mafia, sambamba na Uwanja wa Kaunda- hivi vitu vikiendelezwa,
vitakuwa vitegauchumi vikubwa vya klabu hiyo.
Napongeza
jitihda za Manji kutaka kuujenga upya wa Kaunda na ninasubiri kwa hamu
utekelezaji wake- hiyo itakuwa ni hatua moja kubwa katika kuifanya Yanga
ijitegemee.
Hapa, Yanga
itatengeneza sehemu kubwa ya fedha kutokana na mapato ya milangoni kwa mechi
zake itakazocheza kwenye Uwanja wa Kaunda ukikamilika.
Lakini vipi
kuhusu jengo la Mafia? Au la makao makuu pale Jangwani, kuna mkakati gani wa
kuyaboresha yaweze kuiingizia klabu fedha na kuepuka kuwa tegemeo la mtu au
watu, hao wanaoitwa matajiri?
Tutambue,
Manji si tajiri wa kwanza kutokea Yanga, alikuwepo marehemu Abbas Gulamali.
Tutambue Manji mwenyewe amekwishaingia sana na kutoka Yanga tangu ajitokeze kwa
mara ya kwanza mwaka 2006.
Hata Bin
Kleb mwenyewe amewahi kujiondoa Yanga wakati wa uongozi wa Nchunga- na kwa
sababu hiyo, ni vema kuchukua tahadhari kwa kuwashawishi viongozi wafanye
jitihada za kuifanya klabu ijitegemee.
Lakini pia,
bado kuna mambo madogo madogo katika utendaji, ambayo yanaleta maswali yasiyo
na majibu, mfano nembo ya klabu inavyotumika, je Yanga inanufaikaje?
Watu
wananunua jezi za Yanga, kalenda na bidhaa nyingine, je wanaouza hizi bidhaa
wanailipa klabu? Hili ni suala tu la uongozi kulitolea ufafanuzi na ijulikane
klabu inapata nini na je kinachopatikana ni stahili?
Nilitolea
mfano wa kampuni ya Prime Time Promotions kupewa tenda ya kuandaa mkutano wa
Yanga na kuandaa mechi za kirafiki za klabu hiyo kwa dau la Sh. Milioni 105.
Nikasema,
Yanga ina uwezo wa kuingiza si chini ya Sh. Milioni 300 katika mchezo mmoja tu
wa maana wa kirafiki itakaocheza Uwanja wa Taifa na gharama zote za maandalizi
ya mchezo zisizidi Sh. Milioni 100, iweje mtu apewe tenda kwa bei poa hivyo?
Lakini bado
Yanga ina sekretarieti, viongozi walioajiriwa wanaolipwa na klabu kufanya
shughuli za kila siku za klabu, iweje washindwe kujiandalia wenyewe Mkutano na
mechi za kirafiki?
Kuandaa
mechi ni suala la mawasiliano, Katibu wa Yanga anawasiliana na klabu anazotaka
zicheze na timu yake, wanakubaliana timu inakuja na katika hilo, gharama ambazo
mwenyeji hawezi kuziepuka ni usafiri wa kuja na kurudi kwa wageni, malazi na
usafiri wa ndani.
Maandalizi
ya mchezo- jamani hili pia Katibu wa Yanga hawezi, sasa kaajiriwa kufanya nini?
Mkutano, Yanga ina uzoefu wa kufanya mikutano wa zaidi ya miaka 70 sasa, iweje
leo zoezi hilo anapewa mtu kuratibu?
Nilizungumzia
pia suala la usajili, inaonekana Yanga wanaanza kujisahau baada ya mafanikio
kidogo, kama kutwaa Kombe la Kagame na kuongoza Ligi Kuu baada ya mzunguko wa
kwanza, na sasa kama hawajali hata kufanya usajili makini.
Kumuacha
kipa kama Yaw Berko ili asajiliwe Kabange Twite, kwa kweli binafsi hili ni
jambo ambalo huwezi kumshawishi mtu yeyote mwenye kuelewa soka na uwezo pamoja
na umuhimu wa wachezaji wote hao wawili, akakubaliana na wewe.
Labda
tuambiwe Berko alikuwa ana tatizo lingine. Sitaki kuamini kwamba Yanga wanataka
kushindana tu na Simba, bila hata kujali wananufaika au kuathirika vipi. Nakumbuka,
Mbuyu Twite alikubali kujiunga na Simba bila la sharti la lazima na ndugu yake
asajiliwe, kabla hajabadili mawazo na kusaini Yanga.
Sasa kama
Yanga walipewa sharti na Mbuyu kwamba wakimsajili yeye lazima wamsajili na
ndugu yake, kweli walilitafakari na kukubaliana nalo?
Turudi
kwenye ile timu ya vijana, ambavyo ilianza kufanya vizuri chini ya kocha
Salvatory Edward, je inalelewa vipi hii timu? Kamati ya Utendaji ya Yanga ni
pana sana na bado kuna Kamati ndogo ndogo, hakika wanatosha kwa utekelezaji wa
shughuli za klabu, je wamejigawa vipi na wanatekeleza vipi majukumu yao?
Haya, pamoja
na ukubwa wa klabu, umaarufu, kuwa yenye mvuto mbele ya mamilioni wengi nchini
na hata nchi jirani, iweje hadi leo ina mdhamini mmoja tu Kilimanjaro Beer?
Sekretarieti
ya Yanga imekwishaandika maombi ya udhamini kwenye makampuni mangapi
ikakataliwa?
Yanga ya
sasa ina sura tofauti sana kutokana na aina ya viongozi wake, ina nafasi kubwa
ya kupata wawekezaji zaidi, iwapo italifanyia kazi hilo suala.
Ni kweli
Yanga imepata bahati kubwa kutokana na aina ya viongozi wake wa sasa, lakini
klabu bado haina cha kujivunia. Huo ndiyo msingi wa mada na nitapenda sasa
tujadili hoja ili tupanuane mawazo, pasipo kutukanana. Nawatakia heri ya mwaka
mpya 2013, kiungwana kabisa, naweka.