Na Mahmoud Zubeiry
WADHAMINI wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom Tanzania wametoa
tahadhari kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo, kuendeleza ushindani wa kweli
unaozalisha matokeo halisi ya uwanjani, badala ya kupanga matokeo nje ya Uwanja.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari, mchana huu katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), uliopo ndani ya Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kuhusu
Ligi Kuu, Meneja Mahusiano ya Nje wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Salum Mwalim alisema
kwamba kampuni yake inajisikia fahari kuona soka sasa inachezwa viwanjani zaidi
na si nje.
Akitoa tathmini
yake juu ya mzunguko wake wa kwanza wa Ligi Kuu, Mwalim alisema kwamba ulikuwa
na ushindani mkubwa na umeleta motisha kwa wachezaji mmoja mmoja na hata kwa mashabiki
wa soka nchini.
“Mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom, umeonyesha taswira ya wapi Ligi Kuu ya Tanzania inaelekea,
tumeshuhudia timu kubwa zikienda mikoani zinakabiliana na hali ngumu ya
kiushindani, hazijui zitatokaje. Hicho ni kielelzo cha ushindani,”alisema.
Mwalimu alisema
hata kupanda kwa kiwango cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars pia
ni kielelezo kingine cha kukua kwa Ligi Kuu. “Timu ya taifa imekuwa imara na
hata inapokwenda nje ya nchi, imekuwa inakwenda kushindana, sasa si wasindikizaji
tena,”alisema Mwalim.
Aidha, bosi
huyo Vodacom na mtangazaji wa zamani wa Televisheni ya Channel Ten ya Dar es
Salaam, alisema kwamba imeshuhudiwa pia katika dirisha dogo la usajili timu
zinazoshiriki ligi hiyo zikienda mbio kusaka wachezaji wa kuimarisha vikosi
vyao.
“Hii maana
yake ligi ni ngumu na ya ushindani, kama kungekuwa hakuna ushindani, timu zisingeenda
mbio kuimarisha vikosi vyake,”alisema Mwalim na kuongeza; “Kama wadhamini, hili
linatupa moyo sana, kile ambacho tunawekeza ndani yake tunapata matunda,”alisema.
Mwalim alisema
kwamba soka sasa ni uwekezaji mkubwa katika taifa na ni ajira, wachezaji
wanalipwa vizuri na wengine wananunuliwa na klabu za nje na kupata mikataba
minono.
“Haya yote ni
kielelezo cha ubora wa ligi yetu, kama mtu ananunuliwa nje, maana yake ligi
yetu ni ubora na itazidi kumulikwa,”alisema.
Kuelekea mzunguko
wa pili, Mwalim alisema wanazitakia kila la heri timu zinazoshiriki ligi hiyo
na wananatarajia kuona ushindani ule ule hasa kwa timu za mikoani.
Alisema Vodacom
walikaa pamoja na Kamati ya Ligi Kuu na TFF na kupitia changamoto mbalimbali
ambazo zilijitokeza katika mzunguko wa kwanza na kwamba mambo mengi ambayo yanawahusu
moja kwa moja, wameyafanyia kazi.
“Kabla ya
kuanza mzunguko wa pili, tutangaza mambo mengi mapya kuhusu udhamini wetu, kuna
mambo yanafanyiwa kazi na yanakwenda vizuri, Menejimenti ilikuwa likizo, sasa
wamerudi, wakikamilisha yatatangazwa”alisema.