Umony |
Na Princess Asia
MCHEZAJI
bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Kagame,
Brian Umony amewasili jana kujiunga na timu yake mpya, Azam FC na leo mchana
atakuwamo kwenye msafara unaokwenda Zanzibar kutetea Kombe la Mapinduzi.
Brian alirejea
nyumbani Uganda mwaka jana na kujiunga na KCC baada ya kumaliza mkataba wake
katika klabu ya Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009,
ilikuwa aje kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, lakini Wekundu hao wa Msimbazi
wakazidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Umony
aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya
Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa
mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. kabla ya kurejea Uganda na
sasa anakuja kuanza maisha mapya Azam FC 2013.
Azam
wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro,
Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja,
wakati Kundi A lina timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri
ya Pemba.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo hadi kilele cha miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.