Frank Domayo juzi |
Na Mahmoud Zubeiry
KIUNGO tegemeo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Frank Domayo hana
tatizo zaidi la kiafya, uchunguzi wa Daktari wa klabu, Nassor Matuzya umetoa
majibu hayo.
Yanga iliamua kumfanyia uchunguzi wa afya yake Domayo kutokana
na kusema hupatwa na kizunguzungu mara kwa mara.
Msemaji wa klabu hiyo bingwa Afrika Mashariki na Kati, Baraka
Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, uchunguzi wa Daktari umeonyesha kiungo
hana tatizo na labda alitokewa na mshituko wa kawaida wa mechi Jumapili, kiasi
cha kushindwa kucheza.
Domayo aliyepatwa na hali hiyo ghafla juzi muda mfupi kabla
ya timu hiyo kuingia uwanjani kumenyana na Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, kwa sasa ameruhusiwa kuendelea na mazoezi.
“Kesho ataungana tena na wenzake mazoezini, baada ya Daktari
kuthibitisha huyu mtu hana tatizo lolote,”alisema Kizuguto.
Domayo juzi alizidiwa ghafla Uwanja wa Taifa, akiwa tayari
amefika kwenye chumba cha kubadilishia nguo na amevaa jezi akiwa miongoni mwa
wachezaji 11 waliopangwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kuanza mechi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Yanga lilidhani ni
Malaria na kumkimbiza katika Zahanati ya Uwanja wa Taifa, ambako alipatiwa
huduma ya kwanza na kupata nafuu.
Kwa sababu hiyo, ilibidi nafasi yake aanze kiungo mwingine,
Nurdin Bakari na timu ikafainiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuzidi
kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 32, baada ya kucheza
mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26.