Wacheza wa Toto wakiwa wamembeba kocha wao Athumani Bilal baada ya kuifunga Simba katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kesho watafurukuta Chamazi? |
Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inaingia raundi ya 15 kesho (Januari 30 mwaka huu) kwa
mechi mbili ambapo Azam iliyo katika nafasi ya pili nyuma ya Yanga itakuwa
mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza.
Mechi hiyo
itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam huku Azam ikisaka ushindi ili
kuikaribia Yanga inayoongoza wakati Toto Africans inayonolewa na John Tegete
ikitaka kurekebisha makosa ya kupoteza mechi yake iliyopita dhidi ya Oljoro
JKT.
Uwanja wa
Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro
JKT dhidi ya wageni Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera itakayochezeshwa
na mwamuzi Jacob Adongo wa Musoma.
Ushindi kwa
Oljoro JKT yenye pointi 17 utaihakikishia kubaki katika nafasi yake ya nane
wakati Kagera Sugar inayofundishwa na kocha mkongwe Abdallah Kibaden utaifanya
ipige hatua moja mbele katika msimamo wa ligi.
Ligi
itaendelea tena Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo vinara
Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati
Polisi Morogoro ikiikaribisha African Lyon mjini Morogoro.
Nazo Mgambo
Shooting ya Tanga na Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani zitaoneshana kazi
kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.