Taifa Stars |
Na Prince Akbar
TIMU ya soka
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya
Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Januari 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Stars chini
ya Kocha Mkuu Kim Poulsen inatarajia kuingia kambini jijini Dar es Salaam
keshokutwa (Januari 6 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo. Mechi hiyo itakuwa
kipimo cha mwisho kwa Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
Ethiopia iko
kundi C pamoja na mabingwa watetezi Zambia, Nigeria na Burkina Faso. Ethiopia
itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 mwaka huu dhidi ya Zambia.
Katika mechi
yake ya mwisho, Taifa Stars iliifunga Zambia bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki
uliofanyika Desemba 22 mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo
ya kirafiki dhidi ya Ethiopia ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi
ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014. Mechi hiyo
itachezwa Machi mwaka huu.
Wachezaji
wanaotakiwa kambini ni Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa
Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris
(Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar),
Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni
Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha
(Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa
Sugar).
Washambuliaji
ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa
TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wakati
benchi la Ufundi lina Kim, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali
(Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa
timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Katika hatua
nyingine, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatarajia kukutana leo mchana (Januari 4
mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine itapitia maendeleo ya uchaguzi kwa
wanachama wa TFF ikiwemo Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wanachama wa
TFF (vyama vya mikoa) wote wameshafanya uchaguzi ukiondoa mikoa ya Rukwa na
Katavi inayotarajiwa kufanya uchaguzi baadaye mwezi huu. Kwa upande wa vyama
shiriki ambavyo bado havijafanya uchaguzi ni Makocha (TAFCA), Wachezaji
(SPUTANZA), Waamuzi (FRAT) na Tiba ya Michezo (TASMA).
Vilevile
Kamati ya Uchaguzi ya TFF baada ya kikao hicho huenda ikatangaza rasmi mchakato
wa uchaguzi wa TFF unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.