Ngassa akipiga pushapu za kutambaa baada ya kufunga bao la tatu, aliyesimama jirani yake ni Haruna Chanongo na kushoto ni kipa Abdul Seif akitahari |
Ngassa akiwa amejilaza kwenye nyavu baada ya kufunga. PICHA ZAIDI BAADAYE |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC leo imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-1 African Lyon ya Dar es
Salaam katika mchezo wa ufunguzi wa duru hilo.
Ushindi huo, unaifanya
Hadi mapumziko Simba SC walioweka kambi ya wiki mbili Oman
kujiandaa na mzunguko huu, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyotiwa
kimiani na Mrisho Khalfan Ngassa mawili dakika za 19 na 39 na Ramadhan Suleiman
Chombo ‘Redondo’ dakika ya tatu ya mchezo huo.
Redondo aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tatu,
akiunganisha krosi nzuri ya Ngassa kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti
akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Lyon.
Bao hilo liliwatia chaji Simba SC na kuanza kucheza soka
maridadi zaidi, wakionana kwa pasi za mitindo yote, ndefu, fupi, za juu, chini hadi
visigino na haikushangaza dakika ya 19 walipopata bao la pili.
Ilikuwa ni kazi nzuri ya Ngassa mwenyewe, ambaye baada ya
kupata pasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula aliitoka ngome ya Lyon kabla ya
kumchambnua kipa wa timu hiyo, Abdul Seif.
Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa alikwenda moja kwa moja
kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kukumbatiana na Haruna Moshi Shaaban
‘Boban’ kisha kuwapa mikono wachezaji kadhaa na kurejea uwanjani.
Lyon walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31,
baada ya Shamte Ally Kilalile kukosa penalti.
Refa Israel Mujuni alitoa penalti hiyo baada ya beki Paul
Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis aliyepanda kusaidia mashambulizi, hata hivyo
mkwaju wa kwanza wa Shamte ulipanguliwa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja,
lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai kipa huyo alitokea kabla ya mpira
kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
Simba iliongeza kasi ya mashambulizi ikitumia mipira ya
pembeni, kulia akiteleza Chanongo na kushoto Ngassa, timu ikichezeshwa vyema na
viungo watatu katikati, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude. Ilikuwa
burudani kwa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, kwa jinsi ambayo timu yao
ilitawala mchezo.
Kazi nzuri ya Chanongo aliyeteleza wingi ya kulia huku
akiruka madaluga ya mabeki wa Lyon, iliipatia Simba bao la tatu baada ya krosi
yake nzuri kuunganishwa vyema kimiani na Ngassa.
Baada ya kufunga, Ngassa alishangilia kwa aina yake bao hilo,
kwanza akitambaa hadi langoni na kisha kujilaza kwenye nyavu kubwa kama yeye
ndio mpira.
Baada ya hapo, aliinuka na moja kwa moja kwenda tena kwenye
benchi la wachezaji wa akiba akianza kushangilia na Boban, baadaye wachezaji wengine
na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye alitumia kama sekunde 30 akizungumza
naye jambo.
Kipindi cha pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC
wasiongeze mabao zaidi, huku wao wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi,
lililofungwa na Bright Ike dakika ya 59, pasi ya Fred Lewis.
Dakika ya 64 Ngassa alipoteza nafasi ya kufunga mabao matatu
katika mchezo mmoja, baada ya kukosa penalti.
Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar ililala 1-0 nyumbani mbele ya Polisi Morogoro,
bao pekee la Muzamil Said dakika ya 76, Coastal
Union iliifunga Mgambo JKT 3-1, Ruvu Shooting iliilaza 1-0 JKT Ruvu, bao pekee
la Abdulrahman Seif dakika ya 90 Azam FC imeshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na
JKT Oljoro imeilaza 3-1 Toto Africans.
Ushindi wa
Azam ulitokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 20 na Khamis Mcha
dakika za 31 na 66, wakati la Kagera lilifungwa na Paul Ngway dakika ya 82 na
sasa timu hiyo imejiimarisha katika nafasi ya pili kwa kutimzia pointi 27, sasa
ikizidiwa mbili tu Yanga iliyo kileleni.
Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga mabao ya Coastal yalifungwa na Philip Mugenzi dakika ya 18,
Daniel Lyanga dakika ya 78 na Joseph Mahundi dakika ya 81, wakati la Mgambo
lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 89.
Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mabao ya Oljoro yalifungwa na Hassan Isihaka
dakika ya 15, Paul Nonga dakika ya 51 na 57, wakati la Toto lilifungwa na
Selemani Kibuta dakika ya 73.
Ligi hiyo
itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapomenyana na TZ Prisons kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Kiggi
Makassy, Mussa Mudde/Komabil Keita, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Mwinyi
Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa/Abdallah Seseme, Amri Kiemba na
Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
African Lyon; Abdul Seif, Fred Lewis, Jacob Massawe, Mohamed
Samatta, Abdulaghan Gulam/Hood Mayanja, Yussuf Mlipili, Jackson Kanywa, Aman
Kyata/Yussuf Mgwao, Job Ibrahim, Shamte Ally/Bright Ike na Juma Seif ‘Kijiko’.
MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM
2012/2103:
P W D L GF GA GD Pts
1 Yanga 13 9 2 2 25 10 15 29
2 Azam 14 8 3 3 20 12 8 27
3 Simba SC 14 7 5 2 23 12 11 26
4 Mtibwa Sugar 14 6 4 4 18 13 5 22
5 Coastal Union 14 7 4 3 19 15 4 25
6 Kagera Sugar 14 5 6 3 16 13 3 21
7 Ruvu Shooting 14 7 2 5 20 17 3 23
8 Mgambo JKT 14 5 2 7 11 16 -5 17
9 JKT Ruvu 14 4 3 7 13 21 -8 15
10 JKT Oljoro 14 5 5 5 16 17 -1 17
11 TZ Prisons 13 3 5 5 8 12 -4 14
12 Toto African 14 2 6 6 11 18 -7 12
13 African Lyon 14 2 3 9 10 23 -13 9
14 Polisi Moro 14 1 4 9 5 16 -11 7
MATOKEO
KAMILI MECHI ZA LEO:
Mtibwa Sugar
0-1 Polisi Morogoro
Coastal
Union 3-1 Mgambo JKT
Ruvu
Shooting 1-0 JKT RUVU
Azam FC 3-1 Kagera
Sugar
JKT Oljoro 3-1
Toto Africans
KESHO; Januari 27, 2013
Yanga SC Vs TZ Prisons