Kikosi cha Simba |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
SIMBA SC
inarudi dimbani leo katika Kombe la Mapinduzi, kumenyana na Bandari ya hapa
katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa
kuanzia saa 2:30 usiku.
Simba SC
inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kujihakikishia kutinga Nusu Fainali,
kwani hadi sasa ina pointi nne sawa na vinara wa kundi hilo, Tusker FC ya Kenya
wenye wastani mzuri wa mabao.
Kocha Msaidizi
wa Simba SC, Jamhuri Mussa Kihwelo ameahidi kujiuzulu leo iwapo timu hiyo itafungwa
na Bandari leo.
Katika
mchezo uliopita, Simba SC ilionyesha kuimarika kiuchezaji na kutoa sare dhidi
ya timu ngumu, Tusker ya Kenya ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Amaan
mjini hapa.
Kwenye mchezo
huo, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba
wakitangulia kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi Shaaban, maarufu
kama Boban au Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha dakika ya 39,
mfungaji Khalid Aucho.
Boban
alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu akiwa amedhibitiwa na beki
ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia pasi ya Ramadhan Chombo
‘Redondo’ kuitumbukiza nyavuni.
Baada ya
kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono na kuumia, hivyo hakushangilia bao
lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
Baada ya bao
hilo, Simba iliongeza mashambulizi langoni mwa Tusker na Boban alikaribia
kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache.
Aucho
alifunga bao lake akiunganisha krosi ya Jeremiah Bright kutoka upande wa
kushoto wa Uwanja.
Baada ya
hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza
kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
Kipindi cha
pili timu zote zilirudi vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo
ambalo lilisababisha dakika 90 zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuwa kile kile kilichotoa sare ya
1-1 na Tusker; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Shomary Kapombe,
Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna
Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Julio kushoto akiwa na Kocha Mkuu, Patrick Liewig. Ameahidi kujiuzulu timu ikifungwa |