Kikosi cha Simba kilichotinga Nusu Fainali jana |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
PAMOJA na
kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi jana, Simba SC
italazimika kuiachia timu yao ya pili, maarufu kama Simba B iendelee na michuano
hiyo hata kama ikiingia fainali, ili kikosi cha kwanza kiende Oman keshokutwa.
Kocha Mkuu
wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, anataka
kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza
kuipanga vyema timu yake.
Kuhusu wachezaji
wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na Ethiopia,
Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo. “Najua
viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
Sijui wamekubaliana
vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu Oman baada ya mechi
na Ethiopia,”alisema.
Simba jana
ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari
ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia
kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi
Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa
penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la
hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na
mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi
alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita
20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.
Kipindi cha
pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo,
Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude,
Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao
Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo
hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano
hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama
mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Wachezaji wa
Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari
Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika wachezaji
wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi
ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati
Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu.