Haruna Chanongo aliyeruka kufunga bao la kwanza la Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
MABINGWA wa
Tanzania Bara, Simba SC wameanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya
kuwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri ya Pemba mabao 4-2 usiku huu kwenye
Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Hadi mapumziko,
timu hizo zilikuwa zimekwishafungana mabao 2-2, zikicheza huku zikinyeshewa na
mvua iliyoanza kabla hazijaingia uwanjani.
Jamhuri ndio
waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 17, mfungaji Mfanyeje Mussa Yussuf kwa
shuti la umbali wa mita 17.
Simba
ilisawazisha bao hilo dakika ya 27, mfungaji Haruna Athumani Chanongo
aliyeunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo Kiggi Makassy kutoka
wingi ya kulia.
Baada ya bao
hilo, Simba walizidisha mashambulizi langoni mwa Jamhuri na iliwachukua dakika
mbili zaidi kupata bao la kuongoza, baada ya Chanongo kufumua shuti kali akiwa
umbali wa mita 20 upande wa kushoto mwa Uwanja, ambalo lilimshinda mlinda
mlango Jaffar Said.
Huku ikielekea
kama Simba itatoka uwanjani baada ya ngwe ya kwanza ikiwa inaongoza 2-1, Mfanyeje
tena aliwainua vitini wapenzi wa timu hiyo ya Chasasa, Pemba kwa bao tamu la
kusawazisha akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Abdallah Athumani,
akamtungua kiulaini kipa wa Simba, William Mweta.
Kipindi cha
pili, Simba walirudi kwa kasi ya kusaka bao la ushindi iliwachukua dakika 12 tu
kufanikisha malengo yao, baada ya Nahodha wa timu hiyo leo, Shomary Kapombe aliyecheza
kama kiungo mkabaji badala ya beki wa kati, kufunga kwa shuti la chini la mpira
wa adhabu.
Adhabu hiyo ilifuatia
mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la
hatari na beki mmoja wa Jamhuri.
Sunzu aliwainua
vitini wapenzi wa Simba dakika ya 66, baada ya kuuwahi mpira uliokuwa unaelekea
kutoka nje na kugeuka nao kuutumbukiza nyavuni kiufundi.
Kabla ya mchezo
huo, Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad alizindua
mashindano hayo kwa kupiga penalti na kumfunga kipa wa Jamhuri, Jaffar. Akiongozwa
na raisi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu, Mh Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alizikagua timu zote mbili kabla ya kuanza kucheza.
Kocha mpya
wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alikuwa jukwaani akiishuhudia timu,
ikiongozwa na watakaokuwa wasaidizi wake, Mganda Moses Basena na mzalendo,
Jamhuri Kihwelo.
Katika mchezo
wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema,
Mussa Mudde/Abdallah Seseme dk81, Komabil Keita, Shomary Kapombe, Haroun
Chanongo, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude 67, Felix Sunzu/Ramadhan Singano dk81, Haruna
Moshi na Kiggi Makassy/Christopher
Edward dk27.
Jamhuri FC;
Jaffar Said/Suleiman Maabad dk 75, Msafiri Leonard, Hamad Omar, Hussein Omar, Mfaume
Shaaban, Soud Amoud, Bakari Hamisi, Ally Bilal/Mbara Ali dk82, Ally Ahmed ‘Shiboli’,
Mfanyeje Mussa na Abdallah Athumani.
Katika mchezo
uliotangulia, Tusker ya Kenya iliichapa Bandari ya hapa mabao 5-1, mabao ya Jesse
Were 29 na 43, Ismail Dunga 35 Michael Olunga dakika ya 89 na Andrew Tolowa
dakika ya 90, wakati la Bandari lilifungwa na Amour Janja dakika ya 83.