Na Bin Zubeiry |
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba
SC waliuanza vyema mzunguko wa pili wa ligi hiyo, baada ya kuifunga African Lyon
mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi.
Huo ulikuwa mwanzo mzuri, ingawa matokeo ya mechi nyingine za
Ligi hiyo, ikiwemo Yanga na Azam kushinda kwa idadi sawa na hiyo ya mabao,
yanafanya msimamo wa Ligi Kuu kwa timu tatu za juu ubaki kama ulivyokuwa.
Yanga wenye pointi 32 wanaongoza, wakifuatiwa na Azam wenye
pointi 27, wakati Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 25.
Pamoja na ushindi huo, mashabiki wa Simba walitoka uwanjani
na nongwa ya kutofurahishwa na kiwango cha timu, huku vyombo vya habari
vikiponda timu hiyo ilivyocheza kipindi cha pili.
Katika utetezi, Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
alidai wachezaji waliathiriwa na hali ya hewa ya Dar es Salaam, kwa sababu ya
kukaa kambini Oman kwa wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Haya ya Julio ni blah blah ambazo tumezizoea kuzisikia kutoka
kinywa chake- lakini haizuii ukweli yeye ni kocha na mtaalamu.
Ukweli ambao wana Simba wanapaswa kuuelewa kwa sasa ni
mabadiliko makubwa ndani ya kikosi chao kutoka kile cha msimu uliopita, hasa
katika safu ya ulinzi na hilo limekuwa likiitesa timu hiyo tangu kwenye Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka jana.
Simba wanakabiliwa na changamoto ya kuunda ukuta mpya, baada
ya ule uliowafanya watambe msimu ulipita kutawanyika.
Ukitazama uchezaji wa Simba, kuanzia kwenye safu ya kiungo
kwenda mbele huwezi kuona tatizo na timu inashambulia sana, wanacheza kwa
kuonana na wana wachezaji wenye kasi nzuri tu pale mbele, ukiondoa Mrisho
Ngassa wapo chipukizi kama Ramadhani Chanongo anayeinukia vizuri.
Lakini pia kuna kitu nilikiona ndani ya kikosi cha Simba
ikimenyana na Lyon, ni kama wamebadilisha aina ya uchezaji wao wa taratibu
wakigonga pasi nyingi na sasa wanashambulia kwa kasi kupitia pembeni.
Kwa sababu hiyo, sikustaajabu hata siku hiyo wachezaji wasio
na kasi kama Haruna Moshi ‘Boban’ wakianzia benchi. Aina ya mchezo wanaohamia
Simba SC kwa sasa unahitaji wachezaji kuwa fiti sana ili kuumudu kwa muda wote.
Ndiyo maana nikasema, aliyosema Julio ni blah blah ambazo
tumezizoea, ila ukienda kwenye suala la msingi la kiufundi kwa sasa Simba
inakabiliwa na changamoto ya kutengeneza timu mpya na kuumudu pia mfumo wa
uchezaji wa kasi, ambao inaonekana ndiyo anaoupenda kocha wao mpya, Mfaransa
Patrick Liewig.
Na ndiyo maana utaona aina ya wachezaji waliopangwa kwenye
mechi hiyo wengi ni wenye kasi na hata wale ambao tumezoea kuwaona wakicheza
taratibu, siku hiyo walibadilika kidogo kama Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Kocha ndiye anayeiongoza timu na ndiye anayeamua timu icheze
kwa aina ipi- na kwa aina anayotaka lazima apange aina ya wachezaji ambao
watamudu kuicheza. Amekaa na wachezaji mazoezini kwa wiki takriban tatu kuanzia
Zanzibar na baadaye Oman, amewafundisha na amejua ni akina nani watamfaa katika
kampeni zake.
Hili ni la msingi sana ambalo mashabiki wa Simba kwanza
wanatakiwa walipokee na kulikubali, ikiwa kweli wanataka mabadiliko ndani ya
timu yao. Kwa sasa, naona dalili kama Liewig ataendelea na mfumo huo, timu
itafanya vizuri zaidi kipindi cha kwanza, lakini baadaye wachezaji wakichoka
hali itabadlika.
Hata hivyo, baada ya muda, tena si mrefu iwapo Simba
watavumilia na kocha atapewa sapoti ya kukamilisha mipango yake, timu itakaa
sawa na itakuwa tishio mno kwa mfumo wake.
Tunajua, wapo wachezaji magwiji wa mizengwe, ambao anapotokea
kocha mwenye mazoezi magumu, humfanyia mizengwe ili aondolewe na hili tayari
linamkabili Liewig pale Simba SC na wanaoweza kumuepusha nalo ni viongozi kwa
kuhakikisha wanampa nguvu ya kutekeleza programu yake na kuhakikisha wachezaji
wote wote wanatii.
Kwa lugha nyepesi naweza kusema Simba hivi sasa wanatengeneza
timu, wakiwa tayari wana wachezaji wazuri na hiki ni kipindi ambacho wapenzi wa
timu hiyo wanapaswa kuwa wavumilivu na kuiunga mkono timu yao.
Ingekuwa kazi rahisi kwa Liewig kuisuka upya Simba, kama
angekuta timu ile ile ya msimu uliopita iliyozoeana baada ya kucheza pamoja kwa
muda mrefu, lakini ukitazama kikosi cha kwanza cha Wekundu hao wa Msimbazi kwa
sasa na ukirejea kile kilichotwaa ubingwa msimu uliopita.
Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary
Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto,
Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi- hiki ni kikosi
kilichoichapa Yanga 5-0, leo wangapi wamebaki hapo?
Maftah ameasi kwa sababu anadai haki zake, Yondan amehamia
Yanga, Mafisango amefariki dunia, Uhuru amehamia Azam na Okwi amehamia Etoile
du Sahel ya Tunisia.
Bado hata baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wa akiba kama
Ally Mustafa ‘Barthez’, Obadia Mungusa na Juma Nyosso hawapo kwa sasa. Kama
kukosekana kwa mchezaji mmoja tu kwenye timu kunaweza kuiathiri timu kwa kiasi
kikubwa, amini hata Simba kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuunda
timu mpya.
Tazama kwenye beki pale, hadi sasa bado hawajampata mbadala
wa Yondan, licha ya kujaribu kusajili wachezaji kadhaa, Lino Masombo na Paschal
Ochieng lakini wote wameona hawatafaa.
Wameamua kubaki na Komabil Keita, lakini naye hakubaliki
ndiyo maana kiungo Mussa Mudde amerudishwa kwenye safu ya ulinzi anacheza na
Shomary Kapombe. Hizi ni changamoto ambazo zinaikabili timu hiyo kwa sasa na
mashabiki wanapaswa kuwa waelewa na kuunga mkono jitihada za ujenzi wa Simba
mpya.
Wakishapatikana 11 wa kwanza wa uhakika, watakaocheza kwa
uelewano, mambo mengine yatakuwa madogo tu kama suala la mfumo na kadhalika kwa
sababu timu haiwezi kucheza mfumo ule ule katika kila mechi.
Simba ina wachezaji wazuri sana hadi wale vijana wadogo
waliopandishwa kutoka timu B na wengine wapya ambao bado hawajazoea na ni
wajibu wa mashabiki wa Simba kuwapa sapoti wachezaji wao na si kuanza
kuwakatisha tamaa mapema.
Umefika wakati, mashabiki wa soka nchini waanze kubadilika
taratibu na kuwa waelewa. Kwa sasa jambo la msingi kwa Simba SC ni pointi tatu ili
kujiweka sawa kwenye mbio za ubingwa na bila shaka hilo ndilo lengo la benchi
la ufundi kwa sasa pamoja na changamoto zinazowakabili. Ipo haja ya Simba kuwa wavumilifu kwa sasa,
timu yao ikisukwa upya. Alamsiki.