Wachezaji wa Simba SC |
Na Princess Asia
MABINGWA wa
Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam, baada ya ziara
ya wiki mbili nchini Oman ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Baada ya kuwasili
mchana wa leo, Simba wataingia moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa
kirafiki dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Katika ziara
yake ya Oman, Simba ilipata mechi tatu za kujipima nguvu na kushinda moja na kufungwa
mbili.
Katika
mchezo wake wa mwisho Jumamosi, Simba SC ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Ahly
Sidab kwenye Uwanja wa Sidab mjini Muscat.
Katika
mchezo huo, shujaa wa Simba, alikuwa ni kiungo aliyerudi juu kisoka hivi sasa,
Amri Ramadhan Kiemba aliyeifungia timu hiyo bao la ushindi.
Katika mechi
hiyo nzuri na ya kusisimua, wenyeji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kipindi
cha kwanza, lililofungwa na kiungo Mbrazil, aitwaye Lopez, kabla ya kiungo wa
Simba, Kiggi Makassy kusawazisha kipindi hicho hicho cha kwanza.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na leo Simba walicheza soka
nzuri mno, huku wachezaji vijana, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo
na Shomari Kapombe waking’ara zaidi.
Kipindi cha
pili, kocha Mfaransa, Patrick Liewig alifanya mabadiliko, akiwaingiza Rashid
Ismail, Marcel Kaheza wote waliopandishwa kutoka timu B na Kiemba ambao
waliongeza makali ya Mnyama na hatimaye kupata ushindi huo.
Alikuwa ni
kiungo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga SC, Miembeni na Moro United aliyeipatia
Simba ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman kwa kufunga bao safi la
ushindi dakika za mwishoni.
Katika
mechi nyingine, Simba ilifungwa 1-0 na U23 ya Oman na 3-1 na timu ya Jeshi la
nchi hiyo, Qaboos, bao la Wekundu hao wa Msimbazi, likifungwa na Haruna Moshi
‘Boban’.