Ngassa katikati, kulia Redondo na kushoto Kiemba |
Na Boniface Wambura
MECHI namba 92 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyochezwa
jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi
wa mabao 3-1 dhidi ya African Lyon, imeingiza Sh. 53,756,000.
Watazamaji 9,408 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo
iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000
huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 12,499,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya Uwanja sh.
6,355,806.33, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati
ya Ligi Sh. 3,813,483.80, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh.
1,906,741.90 na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,483,021.48.
Katika mechi hiyo, hadi mapumziko Simba SC walioweka kambi ya
wiki mbili Oman kujiandaa na mzunguko huu, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-0,
yaliyotiwa kimiani na Mrisho Khalfan Ngassa mawili dakika za 19 na 39 na
Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ dakika ya tatu ya mchezo huo.
Redondo aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tatu,
akiunganisha krosi nzuri ya Ngassa kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti
akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Lyon.
Bao hilo liliwatia chaji Simba SC na kuanza kucheza soka
maridadi zaidi, wakionana kwa pasi za mitindo yote, ndefu, fupi, za juu, chini
hadi visigino na haikushangaza dakika ya 19 walipopata bao la pili.
Ilikuwa ni kazi nzuri ya Ngassa mwenyewe, ambaye baada ya
kupata pasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula aliitoka ngome ya Lyon kabla ya
kumchambnua kipa wa timu hiyo, Abdul Seif.
Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa alikwenda moja kwa moja
kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kukumbatiana na Haruna Moshi Shaaban
‘Boban’ kisha kuwapa mikono wachezaji kadhaa na kurejea uwanjani.
Lyon walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31,
baada ya Shamte Ally Kilalile kukosa penalti.
Refa Israel Mujuni alitoa penalti hiyo baada ya beki Paul
Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis aliyepanda kusaidia mashambulizi, hata hivyo
mkwaju wa kwanza wa Shamte ulipanguliwa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja,
lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai kipa huyo alitokea kabla ya mpira
kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
Simba iliongeza kasi ya mashambulizi ikitumia mipira ya
pembeni, kulia akiteleza Chanongo na kushoto Ngassa, timu ikichezeshwa vyema na
viungo watatu katikati, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude. Ilikuwa
burudani kwa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, kwa jinsi ambayo timu yao
ilitawala mchezo.
Kazi nzuri ya Chanongo aliyeteleza wingi ya kulia huku
akiruka madaluga ya mabeki wa Lyon, iliipatia Simba bao la tatu baada ya krosi
yake nzuri kuunganishwa vyema kimiani na Ngassa.
Baada ya kufunga, Ngassa alishangilia kwa aina yake bao hilo,
kwanza akitambaa hadi langoni na kisha kujilaza kwenye nyavu kubwa kama yeye
ndio mpira.
Baada ya hapo, aliinuka na moja kwa moja kwenda tena kwenye
benchi la wachezaji wa akiba akianza kushangilia na Boban, baadaye wachezaji wengine
na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye alitumia kama sekunde 30 akizungumza
naye jambo.
Kipindi cha pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC
wasiongeze mabao zaidi, huku wao wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi,
lililofungwa na Bright Ike dakika ya 59, pasi ya Fred Lewis.
Dakika ya 64 Ngassa alipoteza nafasi ya kufunga mabao matatu
katika mchezo mmoja, baada ya kukosa penalti.
Katika mechi nyingine jana, Mtibwa Sugar ililala 1-0 nyumbani mbele ya Polisi
Morogoro, bao pekee la Muzamil Said dakika ya 76, Coastal Union iliifunga Mgambo JKT 3-1, Ruvu
Shooting iliilaza 1-0 JKT Ruvu, bao pekee la Abdulrahman Seif dakika ya 90 Azam
FC imeshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na JKT Oljoro imeilaza 3-1 Toto
Africans.
Ushindi wa
Azam ulitokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 20 na Khamis Mcha
dakika za 31 na 66, wakati la Kagera lilifungwa na Paul Ngway dakika ya 82 na
sasa timu hiyo imejiimarisha katika nafasi ya pili kwa kutimzia pointi 27, sasa
ikizidiwa mbili tu Yanga iliyo kileleni.
Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga mabao ya Coastal yalifungwa na Philip Mugenzi dakika ya 18,
Daniel Lyanga dakika ya 78 na Joseph Mahundi dakika ya 81, wakati la Mgambo
lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 89.
Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mabao ya Oljoro yalifungwa na Hassan Isihaka
dakika ya 15, Paul Nonga dakika ya 51 na 57, wakati la Toto lilifungwa na
Selemani Kibuta dakika ya 73.
Ligi
hiyo itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapomenyana na TZ Prisons
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.