Waziri Makala akizungumza kushoto na kulia ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah |
Na Mahmoud Zubeiry
SERIKALI imezipa ahueni klabu za Ligi Kuu kwa kupunguza
makato yanayotokana na viingilio vya mechi mbalimbali zinazochezwa kwenye
Uwanja huo na sasa itakuwa inakata asilimia 15 tu baada ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT).
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake asubuhi ya
leo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala alisema kwamba
kuanzia sasa Serikai itakuwa inachukua asilimia 15 ya mapato yote ya mechi
zinazochezwa kwenye Uwanja huo na hakutakuwa na makato mengine yoyote.
Makalla alisema kwamba, awali Serikali ilikuwa inachukua
asilimia 10 ya mapato, lakini kulikuwa kuna makato mengine mengi, kama usafi,
Wachina na kadhalika, ambayo sasa yanaondolewa kabisa.
“Kulikuwa kuna malalamiko ya makato ya Uwanja wa Taifa, serikali
tumelishughulikia. Tulianza kwa vikao, kati yetu serikali, Katibu TFF, BMT, Wakurugenzi
na Kamati ya ligi, ilikuwa ni mijadala mirefu, mwanzoni mambo yalikuwa magumu
kidogo, ila baadaye tukafikia mwafaka,”alisema Makala.
Makala alikumbushia awali Uwanja wa Taifa ulikuwa kwa ajili
ya mechi kubwa, lakini baadaye Simba na Yanga zikaomba zikaruhusiwa. “Ikaja
kuonekana timu zote zinautaka huo Uwanja ndio tukawaruhusu watumie. Tukawa tunafanya
gharama za Uwanja asilimia 20, tunachukua na bado kulikuwa kuna makato mengine
mengi, klabu zikalia lia, tukapunguza hadi ikawa asilimia 10,”alikumbushia.
Makala alisema ili kuondoa dhana ya makato ya kinyonyaji, pande
zote zimekubaliana na kutia saini leo mkataba wa makubaliano mapya ya kutumia Uwanja
wa Taifa.
Aidha, Makala alikumbushia umuhimu wa kuutunza huo kwa sababu
unasifika mno barani Afrika. “Nilipokuwa Nairobi (Kenya), Wakenya watu wa AFC
Leopard walikuwa wanausifia sana Uwanja ule, wanasema ni kati ya viwanja vizuri
sana hapa Afrika, kwa hivyo tuna wajibu wa kuutunza,”alisema.
Alisema mara ujenzi wa Uwanja wa Uhuru utakapokamilika kati
ya Aprili na Juni, mwaka huu matumizi ya Uwanja wa Taifa yatarudi kuwa kama
mwanzo, kwa ajili ya timu za taifa na mechi za wapinzani wa jadi, Yanga na
Simba, wakati mechi nyingine zote zitahamia Uhuru.
Pamoja na utaratibu huo mpya wa makato, Naibu Waziri huyo
alisema kwamba kwa watakaotaka kuukodisha Uwanja kwa shughuli mbalimbali,
watalazimikka kulipia Sh Milioni 20.
Makala pia alisema kwamba serikali imekubali kulipa kodi za
mishahara ya makocha wa timu ya taifa, ambazo zilisababisha akaunti ya Ligi Kuu
ikazuiwa kutokana na ukubwa wa deni hilo la TFF.