Simba SC ya Mapinduzi Cup |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
JAPOKUWA
imepanga kuondoka Jumatano kwenda Oman kwa ziara ya wiki mbili, lakini hadi
unaposoma habari hii, Simba SC haijapokea tiketi za safari hiyo kutoka kwa
wenyeji wao, klabu ya Fanja ya huko.
Makamu Mwenyekiti
wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu
kwamba, wanasubiri kutumiwa tiketi na wenyeji wao hao ndipo watangaze rasmi
ziara hiyo ya Oman.
Kikosi cha
Simba kwa sasa kipo visiwani hapa kikishiriki Kombe la Mapinduzi na tayari kimefuzu
hatua ya Nusu Fainali.
Mapema leo, BIN
ZUBEIRY ilimnukuu Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig akisema
anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza
kuipanga vyema timu yake.
Kuhusu
wachezaji wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na
Ethiopia, Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo.
“Najua viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
Sijui
wamekubaliana vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu
Oman baada ya mechi na Ethiopia,”alisema.
Simba jana
ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari
ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia
kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi
Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa
penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la
hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na
mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi
alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita
20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.
Kipindi cha
pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo,
Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude,
Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao
Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo
hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano
hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama
mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Wachezaji wa
Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe,
viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika
wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza
Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba
ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe
ndipo ajiunge na timu.