Aman Ibrahim Makungu, rais wa ZFA aliyebeba matumaini ya soka ya Zanzibar |
Na Ally Mohammed, Zanzibar
RAIS wa
Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu, ameandika barua ya kutaka
kujiuzulu nafasi yake kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuchoshwa na vitendo vya
baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho cha kukataa mabadiliko chanya.
Taarifa
zilizopatikana kutoka katika chanzo cha kuaminika, ni kuwa barua ya Rais wa Zfa
Taifa iliyoandikwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Zfa Taifa, Kassim Haji Salum,
ambayo imesainiwa na yeye mwenyewe imesema kuwa amechoshwa na tabia ya baadhi
ya viongozi wa juu wa Chama hicho cha kukataa kumpa ushirikiano, huku lawama
nyingi akizielekeza kwa Katibu wake Mkuu na Makano wa Rais kisiwani Pemba
akiwataja kuwa ndio chanzo cha kukosekana ushirikiano katika chama hicho.
Hata hivyo
barua hiyo inatarajiwa kukabidhiwa rasmi keshokutwa mara baada ya kumalizika
kwa ziara rasmi ya Zfa katika wilaya nne za Pemba, ziara ambayo inamalizika
kesho katika wilaya ya Chake Chake.
Hatua hiyo
imekuja kufuatia ziara rasmi ya Viongozi wa ngazi za juu wa Zfa Taifa
wakiongozwa na Rais mwenyewe Aman Makungu, kwenda kisiwani Pemba kwa lengo la
kuzungumza na viongozi wa soka katika wilaya zote za Pemba na ziara hiyo
kudaiwa kususiwa na viongozi wa juu wa Zfa kisiwani Pemba akiwemo Makamo wa
Rais kisiwani Pemba pamoja na Msaidizi katibu wa Zfa kisiwani Pemba.
Katika siku
za hivi karibuni kumekuwa na hali ya kutokuelewana kwa viongozi wa juu wa Zfa
kati ya Unguja na Pemba huku kila upande ukiwa na sababu zake, wakati uongozi
wa Zfa kisiwani Unguja ukilezea tabia ya viongozi wa Kisiwani Pemba kufanya
mambo kienyeji, Uongozi wa Zfa kisiwani Pemba umekuwa ukilalamika juu ya
maamuzi makubwa yanayofanywa na chama hicho bila ya kuwashirikisha huku
wakitolea mfano wa suala la kufungiwa kwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya
Zanzibar 'Zanzibar Heroes'.