Kim Poulsen |
Na Boniface Wambura
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili (Februari 3
mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable
Lions).
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es
Salaam leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa
kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza mechi
ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi
kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya
maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji
wameonyesha wako tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na
Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi
dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema
Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco
na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la
Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast
inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.
Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni
makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki
ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir
Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid
(Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva
(Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam),
Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba).
Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu
wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Katika kikosi hiki, Poulsen hajamuita Jerry Tegete ambaye siku za karibuni amefufua makali yake wakati ameita washambuliaji halisi wawili tu, Ulimwengu na Samatta.