Na Bin Zubeiry |
UKANDA wa
Afrika Mashariki ndio uko nyuma zaidi kimaendeleo katika soka, ukilinganisha na
kanda nyingine barani.
Hakuna nchi
katika ukanda huu imewahi kucheza Fainali za Kombe la Dunia. Imewahi kutokea
kibahati bahati zikashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika, 1988, 1990, 1992 na
2004 kwa Kenya, 1980 kwa Tanzania na 1962, 1968, 1974, 1976 na 1978 kwa Uganda.
Hakuna nchi
iliyowahi kuvuka raundi ya kwanza katika kushiriki kwake fainali hizo, zaidi ya
Uganda pekee ambao walifika hadi Fainali mwaka 1978 nchini Ghana na kufungwa na
wenyeji, Black Stars 2-0.
Nini
matatizo yetu? Ni mengi. Ni msururu. Uongozi mbovu, nidhamu mbovu, kukosa
uadilifu, kukosekana kwa misingi mizuri na kutozingatia utaalamu, hayo kwa
uchache.
Shirikisho
la Soka la Kimataifa (FIFA) limeleta muundo mpya wa Katiba ili kusaidia
kupunguza matatizo ya kiutawala katika ukanda wetu na duniani kwa ujumla,
lakini kwa huku kwetu bado matatizo yapo pale pale.
Watu wamejua
namna ya kupambana na Katiba hizo kwa kubadilisha staili ya vurugu zao. Hivi
kweli yupo mtu anaweza kusema aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd
Baharagu Nchunga alijiuzulu uongozi? Hapana aling’olewa.
Timu
ilifungwa mabao 5-0 na wapinzani wao jadi, Simba SC katika mazingira ambayo
vigumu kuamini ilikuwa kawaida na kana kwamba hiyo haitoshi, alivamiwa na watu
wasiojulikana nyumbani kwake, eti wanaokusudiwa kuwa majambazi kabla ya
kijiuzulu kwake katika kipindi ambacho kulikuwa kuna vita dhidi yake ya kumtaka
aachie ngazi.
Na Simba
nako kuna watu wanapambana kwa sasa kuung’oa uongozi uliopo madarakani chini ya
Mwenyekiti, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye anapambana kiume kuzima jaribio
hilo. Tutauona mwisho wake. Mimi ni mtu ambaye siku zote anaamini, anayeua kwa
upanga, naye atakufa kwa upanga.
Tuachane na
hayo. Desemba mwaka jana, klabu ya Simba ilisaini mkataba mpya na mshambuliaji
wake Mganda, Emmanuel Okwi miaka miwili akichukua kiasi cha fedha kisichopungua
dola za Kimarekani 40,000 na kuongezewa mshahara kwa zaidi ya nusu hadi kuwa
dola za Kimarekani 3,000.
Wakati huo
huo, Simba ilimsajili kipa wa kwanza wa Uganda, Abbel Dhaira kwa dau la dola za
Kimarekani 40,000 miaka miwili na mshahara wa Sh. Milioni 2 kwa mwezi.
Simba ina
Waganda wengine wawili, Kocha Msaidizi, Moses Basena na kiungo Mussa Mudde, na
kwa ujumla Waganda wote hao tayari wameripoti kazini, kasoro mtu mmoja tu,
Okwi.
Ukitazama
mlolongo hapo, Okwi ni Mganda ambaye analipwa zaidi kuliko wenzake wote na hiyo
ni kwa sababu klabu inaujua umuhimu wake, ila ajabu yeye hauthamini umuhimu
wake.
Viongozi
wote wa Simba waliopo hapa Zanzibar wanalalamika wanampigia simu Okwi hapokei.
Hapokei hata siku ya kocha wake, Mganda mwenzake, Basena. Hapokei simu mwezi
mmoja tu baada ya kusaini mkataba mpya uliorutubishwa.
Wakati huo
huo, wapenzi wa soka Afrika Mashariki wanalia kwa nini wachezaji wa ukanda huu
hawawiki Ulaya kama wenzao wa Magharibi, Kaskazini na Kusini. Kama wachezaji
wetu ni aina ya Okwi, kuna ajabu gani!
Bila shaka
mnakumbuka kuhusu Mrisho Ngassa alivyokataa ofa ya kwenda El Merreikh ya Sudan
na huko nyuma alikataa hadi ofa ya kwenda kucheza Ukraine, huyu ndiye mtu
ambaye watu wamemuona anafaa, lakini yeye hana haja.
Naomba
niwape sifa zao kidogo Wakenya, hawa wako tofauti sana na Waganda na Watanzania
na ndiyo maana leo wanajivunia wachezaji kama Dennis Oliech anayechezea Auxerre
ya Ufaransa, Victor Wanyama anayechezea Celtic ya Scotland, McDonald Mariga wa
Inter Milan ya Italia, Kevin Kimani anayechezea Bocholt ya Ubelgiji na Patrick Osiako anayechezea Hapoel
Be'er Sheva ya Israel.
Lakini
ukianzishwa mjadala, wachezaji wa nchi gani kati ya Kenya, Uganda na Tanzania
wana vipaji zaidi- tena uhusishe wataalamu wa soka wa nchi zote, Kenya itakuwa
nyuma kabisa. Ila mafanikio? Kenya itaongoza.
Hakuna siri
nyingine ya mafanikio katika soka zaidi ya nidhamu na kujituma, pamoja na kuwa
na malengo binafsi kwa mchezaji kutaka kufikia kiwango fulani. Haya ni mambo
ambayo wachezaji wa Tanzania na hata Uganda bila shaka wanakosa kwa sasa.
Okwi
amekwishakwenda majaribio zaidi ya mara tatu hadi Ulaya, lakini mwisho wa siku
anarudi hapa hapa Simba SC, tushangae nini akiwa anatudhihirishia nidhamu yake
ni mbovu.
Huyo Hamisi
Kiiza wa Yanga, kama si safari ya Ulaya ya klabu yake, naye vile vile bila
shaka hadi leo angekuwa anasumbuana na timu yake kuwasili mazoezini. Inastaajabisha,
mchezaji klabu inamjali, inamthamini lakini yeye hajali yote hayo na wachezaji
wa aina hii ndiyo kila siku wanafukuzisha makocha.
Hiki ni
kipindi cha klabu kujiandaa kwa ajili ya hatua ya lala salama ya Ligi Kuu na
Ligi ya Mabingwa Afrika ni vizuri kocha akawa na wachezaji wote mazoezini
awaandae kwa pamoja.
Na
ukizingatia Simba imepata kocha mpya, Mfaransa Patrick Liewig, na kwa jumla
benchi zima la ufundi ni jipya, Moses Basena na Jamhuri Kihwelo wote wameanza
kazi hivi karibuni, vema wakawapata wachezaji wote ili wawajue vema waweze
kutengeneza timu yao vizuri.
Lakini si
hivyo, ‘masupa staa’ wanasubiri kuja kuanza kucheza tu, hawataki kuhusika
kwenye programu ya maandalizi, kwa mtaji huu kweli Simba itarudia mambo ya enzi
zile, kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa 1974 au kufika fainali ya Kombe
la CAF mwaka 1993? Tafakari.