Shujaa wa Azam leo, Mwaikimba |
Na Prince Akbar
BAO pekee la
Gaudence Exavery Mwaikimba kwa penalti dakika ya 58, jioni hii limeipa Azam FC
ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwenye
Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Huo ni
ushindi wa kwanza wa Azam katika ziara yake ya wiki moja nchini Kenya, baada ya
jana kufungwa 2-1 na AFC Leopard kwenye Uwanja huo huo wa Nyayo.
Penalti hiyo,
ilitolewa baada ya beki mmoja wa Sofapaka, kuunawa mpira uliopigwa na kiungo
Mkenya, Humphrey Mieno.
Akiuzungumzia
ushindi huo, Kocha wa Azam Muingereza Stewart Hall alisema hii inamaanisha timu
yake sasa imeimarika kiasi cha kutosha na ndiyo maana inashinda mechi hata nje
ya nchi.
Pamoja na
kufungwa jana na Leopard, Azam watajilaumu wenyewe, kwani walipoteza penalti
mbili kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabao ya Leopard
katika mchezo wa jana, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam
lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Salum, Himid Mao/Malika
Ndeule, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika/Luckson Kakolaki, Joackins Atudo, Kipre
Balou/Abdulhalim Humud, Seif Abdallah, Salum Abubakar, Brian Umony/Jabir Aziz, Humphrey
Mieno/Gaudence Mwaikimba na Khamis Mcha/Uhuru Suleiman.
Azam itashuka
dimbani Jumanne, kucheza mechi ya mwisho na timu ya Benki ya Biashara ya Kenya,
KCB kwenye Uwanja wa City na Jumatano watapanda basi lao kuvuka boda la Namanga
kurejea nyumbani Dar es Salaam.