Monja 'Anelka' |
MSHAMBULIAJI
wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Monja Privas Liseki amejiunga na Miembeni ya
Daraja la Kwanza Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili.
Monja yupo
kwenye kikosi cha Miembeni FC kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi visiwani hapa,
ambayo leo usiku itamenyana na Azam FC, ikitoka kuifunga 4-1 Mtibwa Sugar
katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B.
“Nipo hapa
Miembeni, nadhani nitastaafu nikiwa na timu hii. Huku nimekuja kumalizia soka yangu
nafikiri,”alisema Monja alipozungumza na BIN ZUBEIRY leo.
Monja alizaliwa
Agosti 8, mwaka 1975, Kinondoni Muslim mjini Dar es Salaam na alipata elimu
yake pekee, ya Msingi katika shule ya Muhimbili, Upanga mjini Dar es Salaam.
“Mimi nilikuwa napenda sana soka, nilipomaliza shule ya Msingi tu, nikaachana
na shule kabisa nikaanza mitikasi ya soka hadi nikasajiliwa Sigara mwaka 1991
nikiwa bado mdogo sana nina miaka 16 tu,”alisema Monja.
Alicheza Sigara
hadi mwaka 1996 iliposhushwa daraja, akahamia Simba SC ambako alidumu hadi
mwaka 1998 alipotolewa kwa mkopo Yanga ili aichezee kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Hata hivyo,
Monja anasema baada ya kwisha kwa Ligi ya Mabingwa, Yanga walitaka kumsajili
moja kwa moja, ila yeye akakataa na kwenda kujiunga na Mtibwa Sugar ambayo aliichezea
hadi mwaka jana alipotua Miembeni.
“Nikiwa
Mtibwa nilikuwa nikitoka mara moja moja kwenda kubadilisha upepo kwa kucheza Uarabuni
na kurudi Mtibwa, kwa mfano mwaka juzi nilitolewa kwa mkopo niende kuisaidia
Ocean View ya Zanzibar, niliichezea hadi ikachukua ubingwa wa Zanzibar,”alisema.
Mbali na kujivunia
kuwa mchezaji mkongwe zaidi katika soka ya Tanzania, lakini pia Monja
anajivunia kucheza timu ya taifa, kucheza klabu kubwa Simba na Yanga na pia
kucheza soka ya kulipwa Uarabuni.
Katika hayo
amecheza michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Washindi,
Kombe la CAF, Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia katika hatua za
awali za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za michuano hiyo.
“Mimi ndiye
mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kama
utakumbuka Yanga ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza michuano hii. Sasa
mimi nikiwa na Yanga mwaka 1998, wakati huo naitwa Andy Cole kwa jina la utani,
niliifungia Yanga bao katika mechi na Manning Rangers ya Afriika Kusini huu
Uwanja ambao siku hizi mnauita Uhuru, wakati huo unaitwa Taifa. Hiyo mechi
tulitoka 1-1. Nikarudia kufunga tena kwenye mechi na hao jamaa jamaa kwao, siku
wakitufunga 4-1,”alisema.
Monja alisema
kwa sasa anataka aitwe Nicolas Anelka wa Tanzania kwa sababu huyo ndiye
mchezaji mkongwe ambaye anaendelea kucheza soka ya ushindani.
WASIFU WAKE:
JINA: Monja
Privas Liseki
KUZALIWA:
Agosti 8, 1975
ALIKOZALIWA:
Kinondoni
KLABU YA
SASA: Miembeni FC
KUJIUNGA:
2012
KLABU ZA
AWALI:
Mwaka Klabu
1991- 1995 Sigara FC
1996- 1998 Simba SC
1998- 1999 Yanga SC
1999-2012 Mtibwa Sugar