Katibu wa TFF, Angetile Osiah kulia akizungumzia wagombea waliowekewa pingamizi. Kushoto ni Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura. |
Na Mahmoud Zubeiry
WAGOMBEA wote wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu, wamewekewa pingamizi wasigombee
uongozi kwa sababu mbalimbali.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ambaye pia ni Katibu wa
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, amewaambia Waandishi wa Habari mchana huu katika
ukumbi wa Mikutano wa TFF, uliopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwamba, jumla
ya pingamizi 14 zimewafikia tangu Jumatatu wiki hii hadi zoezi hilo linafungwa
jana.
Angetile aliwataja wagombea waliowekewa pingamizi kuwa ni Jamal
Malinzi, Athumani Nyamlani wanaogombea Urais wa TFF, nafasi inayoachwa wazi na
Leodegar Tenga anayeng’atuka, Michael Wambura anayegombea Umakamu, nafasi inayoachwa
wazi na Nyamlani anayehamia kwenye Urais.
Angetile alisema kwamba kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu,
wagombea wa Uenyekiti Yussuf Manji, Ahmad Yahya Juma na Mgombea Umakamu,
Mohamed Said pia wamewekewa pingamizi.
Aidha, wagombea wa nafasi za Ujumbe, Epatha Swai, Eliud Mvella
na Athumani Kambi nao wamewekewa pingamizi.
Nyamlani amewekewa pingamizi mbili, moja na Mtanga Yussuf Gacha
na nyingine ya Menard Justinian, wakati Malinzi amewekewa pingamizi moja na Agape
Fuwe na Wambura ana pingamizi mbili, moja ya Osiah Samuel Msengi na nyingine ya
Saidi Rubeya.
Epatha Swai amewekwa pingamizi na Ramadhan Sesso na Sos Chalamila,
Eliud Mvella amepingwa na Saidi Kiponza, Abdul Changawa na Peter Namengi,
wakati Athumani Kambi amepingwa na Jeremiah John Wambura
Wakati Manji amewekewa pingamizi mbili, na mwanachama maarufu
wa Simba, Daniel Tumaini Kamna na mwanachama wa Yanga, Juma Ally Magoma, Frank Mchaki
amewawekea pingamizi Ahamd Yahya na Mohamed Said.
Angetile amesema Kamati itakutana Jumatano kujadili pingamizi
hizo na amewakumbusha wote waliowekewa pingamizi kufika ofisi za TFF saa 4:00
asubuhi siku hiyo kusikiliza pingamizi zao.