Abeid Mziba |
Na Mahmoud Zubeiry
ABEID Mziba ni miongoni mwa majina yaliyotamba katika soka ya
Tanzania kuanzia miaka ya 1980 hadi 1990 mwanzoni.
Huyu alikuwa mshambuliaji mahiri wa kimataifa wa Tanzania,
aliyewika katika klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
Mziba, alikuwa maarufu zaidi kwa mabao yake kichwa
yaliyomfanya aitwe Tekero, akifananishwa na mganga maarufu wa tiba za kijadi
zamani.
Ukiuliza swali mbele ya mashabiki wengi wa soka nchini, nani
alikuwa mkali wa mabao ya vichwa, jibu litakuwa Mziba Tekero. Kweli jamaa
alikuwa mbaya kwa mabao ya vichwa.
Mziba amefunga mabao mengi sana tangu anaanza soka hadi
anastaafu, lakini yapo mabao 10, ambayo mwenyewe anasema hawezi kuyasahau
milele. Ni yapi hayo? Endelea.
Mziba wa tatu kutoka kulia mstari wa katikati wakiwa katika picha ya pamoja ya kikosi cha Taifa Stars na Waziri Mkuu wa zamani, hayati Rashid Mfaume Kawawa mwenye suti nyeupe |
10. Ilikuwa ni mwaka 1989 katika mchezo wa Ligi Daraja la
Kwanza, sasa Ligi Kuu Yanga ilipomenyana na Ushirika mjini Moshi, Mziba
aliifungia timu yake bao pekee la ushindi dakika ya 75 akiunganisha kwa kichwa krosi
ya Kenneth Mkapa. Anasema analikumbuka bao hilo, kwa sababu Yanga ilivunja
rekodi ya Ushirika kutofungwa kwenye Uwanja wao.
9. Ilikuwa ni mwaka 1983 Yanga ilipomenyana na Reli mjini Morogoro
Mziba alipofunga bao pekee la ushindi Uwanja wa Saba Saba, akiunganisha kwa
kichwa kona ya Yussuf Ismail Bana dakika ya 77. Anasema analikumbuka bao hilo
kwa sababu wakati huo Reli ilikuwa moto na haifungiki kwa urahisi, hadi ikaitwa
Kiboko ya Vigogo, lakini yeye alizima ngebe zao.
8. Ilikuwa ni mwaka 1984, Yanga ilipomenyana na Coastal Union
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa 2-0, Mziba akifunga bao
la pili dakika ya 81 kwa shuti la umbali wa mita 40, baada ya kutengewa pasi na
Charles Boniface Mkwasa. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu kwanza alifunga
kwa mguu na tena kwa shuti la mbali, lakini pia lilikuja kuwazima Coastal waliokuwa
wanasaka bao la kusawazisha.
7 Ilikuwa ni mwaka 1987, wakati Yanga ilipokutana na Simba
katika mchezo wa ligi pia, Mziba alipoifungia timu yake bao pekee la ushindi
dakika ya 47, akimalizia pasi ya Yussuf Bana na kumchambua kipa Moses Mkandawile. Anasema analikumbuka bao hilo kwa
sababu lilikuwa tamu na liliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi msimu huo.
6.Ilikuwa mwaka 1989 Yanga ilipokutana na Simba katika mchezo
wa Ligi Kuu na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Mziba akifunga bao la ushindi
dakika ya 85, baada ya kuwapunguza mabeki wa Simba, Twaha Hamidu, Raphal Paul,
Frank Kasanga Bwalya na Iddi Suleiman ‘Meya’ kisha kumtungua kipa Moses Mkandawile.
Anasema analikumbuka bao hilo, kwa sababu lilikuwa tamu akiwapunguza mabeki,
lakini pia alilifunga dakika tano tu tangu aingine uwanjani kuchukua nafasi ya
Mohamed Kiboroga.
5. Ilikuwa ni mwaka 1989, Yanga ilipokutana na African Sports
ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mziba alipoifungia Yanga bao la
kufutia machozi ikilala 2-1. Anasema alifunga
bao hilo dakika ya 70 na mabao yote ya Sports yalifungwa na marehemu Victor
Mkanwa. Anasema analikumbuka bao hilo, kwa sababu wakati huo Sports ilikuwa ina
ukuta mgumu.
4. Ilikuwa ni mwaka 1985 wakati Yanga ilipokutana na Simba SC
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoka sare ya bila kufungana mechi
ikivunjika dakika ya 88. Mziba anasema siku hiyo alifunga bao lililoelekea kuwa
la ushindi, lakini beki wa Simba SC, Talib Hilal akautoa mpira nyavuni kwa
mkono, ila refa alipoamuru penalti, Simba wakagomea mchezo na mechi ikaishia
hapo. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu japo lilikataliwa lakini lilikuwa
halali na Zaidi lilivunja mechi.
3. Ilikuwa ni mwaka 1987, Yanga ilipokutana na Small Simba katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Muungano, Uwanja wa Amaan, Zanzibar na kuibuka na ushindi
wa 1-0, bao pekee la Mziba dakika ya mwisho kati ya tatu za za majeruhi,
akiunganisha pasi ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na kuiwezesha Yanga kutwaa
ubingwa wa michuano hiyo mwaka huo. Anasema analikumbuka bao hilo, kwa sababu
wakati huo Small Simba ilikuwa tishio na kuifunga Uwanja wa Amaan ilikuwa
vigumu.
2. Mwaka 1987 tena katika Ligi ya Muungano, Mziba aliifungia
Yanga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Malindi, akiunganisha krosi ya
Freddy Felix Minziro dakika ya 70. Bao la kwanza la Yanga, alifunga Minziro na Mziba
anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu Malindi ilikuwa tishio wakati huo.
1 Ilikuwa ni mwaka 1984 katika michuano ya Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Mziba alipoifungia Bara, siku
hizi Kilimanjaro Stars bao la kusawazisha dakika ya 65 dhidi ya Uganda, The
Cranes kwenye Uwanja wa City, Nairobi akiunganisha pasi ya Willy Kiango, timu
hizo zikitoka 1-1. Anasema analikumbuka bao hilo, kwa sababu wakati huo Uganda
walikuwa wana ukuta mgumu sana, lakini yeye aliweza kuupenya na kufunga. Na anasistiza
haikuwa kazi nyepesi.
Naam, hayo ndiyo mabao 10 kati ya mengi aliyowahi kufunga
Mziba enzi zake ambayo anasema hawezi kuyasahau.
WASIFU WAKE:
JINA: Abeid Mohamed Mziba
KUZALIWA: Februari 12, 1962
ALIPOZALIWA: Ujiji, Kigoma
TIMU ALIZOCHEZEA:
Mwaka Timu
1975- 1977 Ufundi
Kigoma
1978- 1979 Reli
Morogoro
1979-1980 Reli
Dodoma
1980-1992 Yanga
SC
Amecheza timu ya taifa, kuanzia mwaka 1980 hadi 1989.
Abeid Mziba |