Malinzi akiwa na swahiba wake Matandika |
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(4) katika
kikao chake kilichofanyika tarehe 30 Januari 2013, ilijadili pingamizi
zilizowekwa dhidi waombaji uongozi wa TFF na TPL Board na kutoa maamuzi kama
ifuatavyo:
1. Waombaji uongozi wa TPL Board
(a) Pingamizi dhidi ya Ndg. Said
Muhammed Abeid anayeomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi
(TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya Ndg. Said
Muhammed, aliyeoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kumwondoa mwombaji uongozi kugombea nafasi aliyoomba, kwamba Ndg. Said
Muhammed:
(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya
Azam na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.
(ii) Si mkweli katika maelezo
aliyoyatoa kwenye fomu yake ya maombi ya uongozi.
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mweka pingamizi na ilijiridhisha kuwa
pingamizi iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Mchaki haikukidhi matakwa Kanuni
za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa haikuambatanishwa na vielelezo
vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa
pingamizi hiyo.
(b) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Yusufali Manji anayeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL
Board): Kamati ilijadili pingamizi zilizowasilishwa na
Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg. Juma
Ally Magoma walioomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kumwondoa mwombaji uongozi kugombea nafasi aliyoomba, kwamba Ndg.
Yusufali Manji :
(i) Hana uzoefu wa uendeshaji wa
Mpira wa Miguu uliothibitishwa wa angalau miaka mitano (5) wa uendeshaji wa
mpira wa miguu.
(ii) Hana sifa ya kuwa ama mchezaji
Mpira wa Miguu, Kocha, Mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa Mpira wa Miguu
katika ngazi ya Mkoa au Ligi daraja la kwanza.
(iii)
Hana elimu ya kidato cha
nne
(iv) Ameshindwa kusimamia katiba ya
Young Africans Sports Club Ibara ya 10(6), 18(1)b, 27 (2) na (5).
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa pingamizi
zilizowasilishwa mbele yake na Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg. Juma Ally Magoma
hazikukidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa
hazikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imezitupa pingamizi hizo.
(c) Pingamizi dhidi ya Ndg. Hamad
Yahya Juma anayeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board):
Kamati ilijadili pingamizi iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya
Ndg. Hamad Yahya Juma, kwamba Ndg. Hamad
Yahya Juma:
(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya
Mtibwa na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.
(ii) Si mkweli na mwadilifu na
amekuwa akijipachika cheo cha mwenyekiti wa klabu.
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imeitupa pingamizi ya Ndg. Frank M. Mchaki kwa kuwa pingamizi
iliyowasilishwa mbele yake haikukidhi matakwa
ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na
vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.
2. Waombaji uongozi wa TFF
(a) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Athumani K. Kambi anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF kupitia Kanda ya 9 (Mtwara na Lindi): Ndg. Kambi aliwekewa pingamizi kwamba
amefanya Kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Kamati
imeitupa pingamizi ya Ndg. Jeremiah John Wambura kwa kuwa mweka pingamizi
hakutokea wakati alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi kutoa utetetezi
wake kuhusu pingamizi.
(b) Pingamizi dhidi ya Ndg. Eliud
P. Mvella anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
kupitia Kanda ya 7 (Iringa na Mbeya): Ndg. Mvella aliwekewa pingamizi na Ndg.
Said Kiponza, Ndg. Abu Changawa na Ndg. Peter Naminga, kwamba Ndg. Mvella:
(i) Akiwa mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF kupitia Kanda hiyo ameshindwa kuleta maendeleo ya soka katika
ukanda huo.
(j) Ana kesi ya rushwa katika
mahakama ya wilaya ya Iringa
Kamati
imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za
TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha
maelezo ya pingamizi.
(c) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Epaphra Swai anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
kupitia Kanda ya 3 (Shinyanga na Simiyu): Kamati ilijadili pingamizi
zilizowasilishwa na Ndg. Ramadhani Sesso na Ndg. Tsotsie Chalamila, kwamba Ndg.
Epaphra Swai:
(i) Alifanya ubadhilifu wa fedha
alipokuwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA).
(ii) Alitumia madaraka yake vibaya
alipokuwa MZFA kujinufaisha kwa kutumia MZFA.
(iii) Alivunja Katiba ya MZFA na FIFA
(iv) Anavuruga shughuli za uendeshaji
mpira wa miguu mkoani Simiyu.
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa wawekaji
pingamizi hawakuwa na sababu za msingi zilizoambatana na vielelezo
vinavyothibitisha maelezo ya pingamizi na kuwa pingamizi zilizowasilishwa mbele
yake zina chembechembe za wazi za mapatano ya hila na udanganyifu (collusion)
dhidi ya Ndg. Epaphra Swai. Kwa kutokidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF
Ibara ya 11(2) na hila/udanganyifu kwa Kamati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
imezitupa pingamizi hizo.
(d) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Vedastus F.K Lufano na Ndg. Mugisha Galibona wanaoomba kugombea nafasi ya
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 2 (Mwanza na Mara): Ndg.
Lufano na Ndg. Galibona waliwekewa pingamizi
na Ndg. Paul Mhangwa kwamba
hawana uzoefu wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu wa miaka mitano (5).
Kamati
imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara
ya 11(2).
(e) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Michael R. Wambura anayeomba kugombea nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF:
Pingamizi ziliwasilishwa na Ndg. Said Rubea Tamim na Ndg. Josea Samuel Msengi
kwamba Ndg. Wambura:
(i) Alikiuka Katiba ya TFF kwa
kuishitaki Klabu yake ya Simba mahakamani kuhusu masuala ya uchaguzi.
(ii) Alikosa uadilifu kwa kutumia
kampuni yake binafsi kufanya biashara na Taasisi aliyokuwa aniongoza akiwa
Katibu Mkuu wa FAT.
(iii) Amekuwa akijaribu kupotosha
umma kwamba vyombo vya TFF havifanyi kazi zake kwa kutumia haki na kuviita
‘Mahakama za Kangaroo (Kangaroo Courts).
(iv) Mwaka 2004 alikiri kwamba
alikuwa akiandikwa vizuri na vyombo vya habari kwa kuwa alikuwa akivipa pesa na
kwamba vyombo vya habari vilimgeuka kwa sababu aliacha kuwapa waandishi pesa.
(v) Mwaka 2004 alikataa kutekeleza
maagizo ya FIFA ya kutaka nafasi ya Katibu Mkuu wa FAT iwe ya kuajiliwa.
(vi) Alikosa uwezo wa kutekeleza
wajibu na malengo ya TFF.
Ndg. Josea
Samuel Msengi aliondoa pingamizi lake dhidi ya Ndg. Wambura. Kamati imelitupa
pingamizi la Ndg. Said Rubea Tamim kwa kuwa halikukidhi matakwa ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2).
(f) Pingamizi dhidi ya Ndg. Jamal
E. Malinzi anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF; Aliwekewa Pingamizi na
Ndg. Agape Fue kwamba:
(i) Alivunja Katiba ya TFF kwa
kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa wanachama wa TFF kikiwemo Chama
chake cha Mkoa wa Kagera haviheshimu wala kutekeleza maagizo ya TFF, CAF,
CECAFA na FIFA baada ya Kamati ya Utendaji ya TFF kuwasilisha mapendekezo ya
mabadiliko ya Katiba kwa njia ya Waraka, ambayo yalihusisha pia maagizo ya FIFA na CAF
(ii) Hana sifa ya uzoefu wa miaka
mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
(iii) Anakosa uadilifu na haiba ya
kuliwakilisha Shirikisho nje na ndani.
Kamati
imeitupa pingamizi ya Ndg. Agape Fue kwa kuwa mweka pingamizi hakutokea wakati
alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi kutoa utetetezi wake kuhusu
pingamizi hilo.
(g) Pingamizi dhidi ya Ndg.
Athumani J. Nyamlani anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF: Ndg. Nyamlani
aliwekewa pingamizi na Ndg. Mintanga
Yusuph Gacha na Ndg. Medard Justiniani kwamba:
(i) Ni Hakimu Mkazi katika
Mahakama ya Tanzania na kwa maana hiyo ni mtumishi wa umma hivyo alikosa kigezo
na sifa ya kugombea nafasi ya urais wa TFF.
(ii)
Anakatazwa na Judicial
Service Act, Public Service Act 2002 na Code of Conduct for Judicial Officers
of Tanzania kugombea nafasi aliyoomba ya Rais wa TFF.
(iii) Kutakuwa na Mgoganao wa
kimaslahi endapo Ndg, Nyamlani atachaguliwa kuwa Rais wa TFF.
(iv) Amekosa umakini na uadilifu kwa
kushindwa kutekeleza wajibu wake na kusababisha Akanunti za TFF kufungiwa na
TRA.
Ndg.
Mintanga Yusuph Gacha hakufika kutetea Pingamizi lake ni hivyo halikujadiliwa
na Kamati. Kamati imelitupa pingamizi la Ndg. Medard Justiniani kwa kuwa
alishindwa kuithibitishia Kamati kuwa alikuwa na ufahamu wa kutosha wa
pingamizi lake ikiwa ni pamoja na viambatanisho vyake, hali iliyotanabaisha
kuwa pingamizi hilo lilikuwa na chembechembe nyingi za hila na udanganyifu.
Angetile
Osiah
KATIBU
KAMATI YA
UCHAGUZI