Wachezaji wa African Lyon |
Na Boniface Wambura
KLABU ya African Lyon ndiyo klabu iliyoongoza kwa kusajili
wachezaji wengi kwenye dirisha dogo kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu
ya Vodacom utakaotoa bingwa wa Tanzania Bara, lakini pia timu tatu ambazo msimu
ujao zitarudi kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kati ya wachezaji 65 waliotua katika klabu mbalimbali katika
dirisha hilo, Lyon ndiyo iliyoongoza kwa kuwanasa 12. Miongoni mwao hao, wawili
(Ibrahim Job na Shamte Ally) imewachukua kwa mkopo kutoka Yanga.
Pia watano imewapandisha kutoka katika kikosi chake cha U 20.
Wachezaji hao ni Nurdin Musa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman
Kajembe na jarufu Kizombi. Wengine walioingia katika timu hiyo katika dirisha
dogo ni Juma Seif (Huru), Buya Jamwaka (Burkina Faso), Takang Valentine (Huru)
na Yusuf Mgwao (Huru).
Nayo Polisi Morogoro katika kuhakikisha inaondoka mkiani mwa
ligi imesajili wachezaji wanane katika dirisha dogo kama ilivyofanya Oljoro JKT
ya Arusha.
Wachezaji wa kigeni walioingia katika dirisha dogo ni
Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo (Azam), Donald Obimma na Ulugbe
Chika (Toto Africans), Zuberi Hamis na Tinashe Machemedze (Coastal Union), Musa
Mudde na Abel Dhaila (Simba).
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa
wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo
timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa katika viwanja sita tofauti.
Mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon
katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka Oman
kwenye ziara ya mafunzo.
Pia Kocha wake mpya, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa
mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses
Basena na Jamhuri Kihwelo.
Mwamuzi wa kimataifa Israel Mujuni ndiye atakayechezesha
mechi hiyo ambapo African Lyon inatarajiwa kuongozwa na Kocha Charles Otieno
baada ya kusitisha kibarua cha Pablo Velez kutoka Argentina kutokana na kufanya
vibaya katika mzunguko wa kwanza.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo
wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi
Morogoro na wenyeji Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika
msimamo wa VPL ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Coastal Union ambayo kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji
sita akiwemo Mzimbabwe Tinashe Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao
Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Timu zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT
Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani
ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa
refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho,
Azam baada ya mechi za kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya
Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja
wa Chamazi.
Ni mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala
bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana
Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Maafande wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao
katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.
Yanga iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili
mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons
katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Vinara hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi
ya Azam wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo
kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.
Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza
iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya
washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.
Wakati ameingiza wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha
wa Tanzania Prisons, Jumanne Chale amempoteza David Mwantika katika dirisa
hilo. Beki huyo ametua katika timu ya Azam.