Na Bin Zubeiry |
KUNA mijadala huibuka na kujirudia na kujirudia kuhusu
wachezaji wa kizazi cha sasa na wale wa vizazi vilivyopita, wapi ni bora zaidi.
Mara nyingi wachezaji wa zamani humwagiwa sifa na wa sasa
hukandiwa si lolote, watu wanakumbuka zamani, wanasema wakati huo ndipo soka
ilikuwa inapambwa na wachezaji wa ukweli.
Sitaki kupingana na hili, lakini naweza tu kulijadili kwa
kina suala hili, nini tatizo la wanasoka wa leo au soka yetu kwa ujumla?
Bahati nzuri nimeanza kuwa karibu na viongozi wa soka na
wachezaji tangu miaka ya 1990, wakati naanza kuandika habari za michezo,
kuanzia gazeti la Mfanyakazi, baadaye Dimba ambako nilistaafu Mei mwaka jana na
kuwa mwandishi wa kujitegemea.
Nimejifunza mengi sana juu ya wachezaji na viongozi kwa
ujumla wa wakati huo na wa sasa na kwa muhtasari naweza kusema kuna tofauti
kubwa, ambayo inasababishwa na mambo mengi, kubwa ni aina ya viongozi wa sasa.
Viongozi wa sasa ni tatizo kubwa, wengi wapo kwa maslahi yao
binafsi, kuitumia soka kujinufaisha kwa kipato na kusaka umaarufu.
Miaka ya nyuma, fedha haikuwa kigezo cha mtu kupewa uongozi
haswa katika klabu za Simba na Yanga- kama mtu ana fedha na anapenda timu
anaweza akawa mfadhili tu na kupewa heshima kubwa, lakini suala la uongozi
lilikuwa lina watu wa aina yake.
Hatukuwa na viongozi wasomi sana, na wengine hawakuwa na
elimu ya darasani kabisa, lakini waliweza kuongoza soka, kuwaheshimu wachezaji
na kuishi nao vizuri.
Kuna wakati, Edibily Jonas Lunyamila akiwa juu sana soka,
aliendelea kuichezea Yanga chini ya Mwenyekiti Rashid Ngozoma Matunda (sasa
marehemu), na japo hakuwa na fedha wala shule.
Mzee Matunda alikuwa ana hekima na busara na alijua namna ya
kuishi na wachezaji na ndio maana Lunyamila alijisikia raha kuicheza Yanga japo
haikuwa na fedha. Chini ya Matunda, Yanga iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza
nchini kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Najaribu kukumbuka namna wachezaji wa wakati ule walivyokuwa
wanathaminiwa na viongozi wao, wanaheshimiwa na hiyo ilikuwa moja ya sababu ya
wao kucheza muda mrefu.
Madaraka Suleiman aliyeanza kucheza soka miaka ya 1970
aliichezea Simba hadi mwaka 2003 akiwa mtu mzima sana- kwa nini? Viongozi wa
wakati huo walimheshimu na wakajua namna ya kumtumia licha ya umri wake mkubwa
sana wakati huo.
Lakini Said Maulid ‘SMG’ aliyeanza kucheza Ligi Kuu mwaka
2000 katika klabu ya Simba, kabla ya 2001 kuhamia Yanga, alikocheza hadi 2007
alipohamia Angola, sasa Yanga hawataki hata kumsikia.
Baada ya kumaliza mkataba wake Angola, mwishoni mwa mwaka
jana, SMG aliomba amalizie soka yake Yanga, klabu aliyoichezea kwa mapenzi yake
yote, lakini hakupewa nafasi hiyo. Na mbaya zaidi alifanyiwa dharau sana.
Mussa Hassan Mgosi aliyeanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2001 pia,
alitamani sana baada ya kumaliza mkataba
wake DRC amalizie soka yake Simba SC, klabu aliyoitumikia kwa mapenzi yake
yote, lakini hakuipata nafasi hiyo.
Emmanuel Gabriel na Ulimboka Mwakingwe waliachwa Simba eti
wamekuwa wazee, lakini klabu baadaye ikamsajili mchezaji ambaye labda ni rika
la akina Jamhuri Kihwelo, Paschal Ochieng.
Viongozi wengi wa kisasa wanawadharau sana wachezaji. Kuna
kiongozi mmoja wa Simba, alimkandia Uhuru Suleiman, eti hawezi kupata namba
hata TASWA, ile timu ya Waandishi wa Habari za michezo, lakini bahati yake
kiungo yuyo sasa hivi yupo Azam.
Kwenye Katiba zetu, katika kanuni za uchaguzi kuna kipengele
cha uzoefu wa mgombea kabla ya kugombea uongozi katika ngazi za juu, lakini
umekuwa ukitumika ujanja ujanja tu kupitisha watu ambao hawana uzoefu na
madhara yake ndiyo haya, tunaingiza watu mafedhuli, wajivuni, washamba wanakuja
kutuharibia soka yetu.
Watu wanajifanya wajuaji, wakati hawajui lolote na wanazitia
hasara za mamilioni hata kampuni zao kwa ujuaji wao. Watu wenye tamaa ya fedha,
wanafikiria fedha tu. Wanataka kupata fedha nyingi na utajiri wa haraka haraka
kupitia mpira. Tatizo sana.
Inawezekana kabisa mchezaji wa Tanzania wa leo akacheza hata
miaka 20, iwapo atakuwa chini ya viongozi wadilifu, wenye busara na kuijua
soka. Siyo hawa watafuta maisha wa leo.
Mchezaji amekwishatumika mathalani miaka nane, kuna namna
yake ya kumtumia ili acheze muda mrefu. Huyo hata mazoezi yake ni tofauti na
wachezaji chipukizi. Hassan Afif alikuwa mtu mzima na kibonge mwaka 1991 akiwa
kocha mchezaji Simba na kuiwezesha timu kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, tangu 1974.
Alikuwa akiingia kutokea benchi, anakwenda kuiongoza timu
vema na mara nyingi alikuwa chachu ya ushindi. Hata matokeo yakiwa 0-0, enzi
zile akiinuka tu Afif, jukwaa linaripuka kwa shangwe, wanajua mabao yanakuja.
Vipi leo?
Ni kweli kuna wachezaji mafedhuli, hao walikuwepo tangu
zamani, lakini bado tuna tatizo la viongozi ambao hawajui namna ya kuishi na
wachezaji.
Viongozi wanawakatisha tamaa wachezaji, tena sana. Hivi SMG
kama angesajiliwa Yanga au Mgosi Simba, wangezipunguzia nini klabu kama si
kuzinufaisha kwa uzoefu wao? Samahani wapendwa wasomaji wangu, pamoja na yote
niliyoeleza lakini naongeza kuna watu waliopewa mamlaka kwenye klabu wana roho
mbaya!
Wakati mwingine wachezaji wanadai haki zao za msingi, tena
zilizomo kwenye mikataba matokeo yake wanaitwa watovu wa nidhamu na wanafukuzwa
kwenye timu.
Anayefanya hivyo hajali uwezo wa mchezaji na mchango wake
kwenye timu, je kwa mtaji huu tutafika kweli? Naungana na mawazo ya mengi,
wachezaji wa ukweli walikuwa zamani, lakini hata wa sasa wanashindwa kufikia
kiwango cha wachezaji wa zamani kwa sababu ya kukwazwa na viongozi wetu wa leo.
Alamsiki.