Simba na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya 1-1 |
Na Mahmoud Zubeiry
MZUNGUKO wa
pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unatarajiwa kuanza leo, nyasi za
viwanja sita tofauti nchini zikiwaka moto katika mechi za ufunguzi za mzunguko
huo wa lala salama.
Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam,Watoto wa Zamunda, African Lyon watamenyana na mabingwa
watetezi, Simba SC wakati Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar
watakuwa wenyeji wa Polisi ya Morogoro mjini.
Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT wakati Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting watawakaribisha ndugu zao, JKT Ruvu,
huku Azam FC wakiwa wenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, JKT Oljoro
wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza.
Vinara wa
Ligi hiyo, Yanga SC wao wataanza mbio za kurejesha taji Jangwani keshokutwa,
watakapomenyana na Maafande wa jeshi la Magereza, Prisons kutoka Mbeya.
Je, timu
zinaingia kwenye mzunguko wa pili zikiwa katika nafasi gani na zimejiandaaje
kuelekea hatua hiyo ya lala salama? Endelea.
YANGA SC:
Walimaliza
mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu, wakiwa na pionti zao 26, baada
ya kucheza mechi 13, kufungwa mbili dhidi ya Mtibwa Sugar 3-0 na Kagera Sugar
1-0, zote ugenini, kutoa sare mbili 1-1 dhidi ya Simba SC na 0-0 dhidi ya
Prisons.
Yanga ambayo
msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu Ligi Kuu, ilipanda kileleni Novemba 4,
baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 na kuwashusha mabingwa watetezi,
walioongoza ligi hiyo tangu mwanzoni.
Katika ya
mzunguko wa kwanza, Yanga ilifikia kuzidiwa pointi saba na Simba lakini Oktoba
31, ikafanikiwa kuwafikia Wekundu hao wa Msimbazi, siku hiyo wao wakiifunga
Mgambo JKT 3-0 Dar es Salaam na wapinzani wao0 wakilazimishwa sare ya bila
kufungana na Polisi Morogoro.
Baada ya
mapumziko mafupi, Yanga walianza kujifua Dar es Salaam, kabla ya kwenda kwenye
ziara ya mafunzi Uturuki kwa wiki mbili ambako pamoja na mazoezi walipata mechi
tatu za kujipima nguvu na waliporudi, pia wamecheza mechi mbili za kujipima nguvu
dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, ambazo wameshinda zote. Katika dirisha
dogo, Yanga imeongeza mchezaji mmoja tu, Kabange Twite kutoka APR ya Rwanda.
P W D L GF GA GD Pts
1 Yanga 13 9 2 2 25 10 15 29
KOCHA; Ernie
Brandts (Uholanzi)
Ilimaliza
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili, kwa pointi zake 24,
ikiwazidi pointi moja tu mabingwa watetezi, Simba SC. Azam walikuwa na mwelekeo
wa kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kama si kufungwa mechi mbili mfululizo za
mzunguko wa kwanza, dhidi ya Yanga 2-0 na Mgambo JKT 2-1.
Azam ilianza
vema tu ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba tangu mwanzo hadi Oktoba 31,
ilipoenguliwa na Yanga katika nafasi ya pili. Ikielekea kwenye mechi yake ya
mwisho dhidi ya Mgambo, Azam ilifukuza wachezaji wake wanne, Deo Munishi
‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa madai walipokea hongo
waifungishe timu hiyo dhidi ya Simba na wanadai wana ushahidi hadi wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Dhahiri kuondolewa kwa wachezaji
hao tegemeo kikosini kulichangia matokeo ya kufungwa na Mgambo katika mechi ya
mwisho.
Baada ya
mapumziko mafupi, Azam ilianza kujifua tena na ikaenda Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) kucheza Kombe la Hisani, walilofanikiwa kutwaa. Waliporudi
wakaenda kwenye Kombe la Mapinduzi, ambako pia walitwaa taji hilo. Baada ya
hapo, wakafanya ziara ya wiki moja Kenya, ambako walicheza mechi tatu za
kujipima nguvu, wakishinda mbili na kufungwa moja.
Katika
dirisha dogo, Azam imesajili wachezaji saba, ambao ni Humphrey Mieno kutoka
Kenya, Brian Umony (Uganda), Jockins Atudo (Kenya), David Mwantika (Prisons),
Abdallah Seif (Ruvu Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani kwa
mkopo kutoka Simba SC.
P W D L GF GA GD Pts
2 Azam 13 7 3 3 17 11 6 24
KOCHA:
Stewart Hall (Uingereza)
SIMBA SC:
Mabingwa hao
watetezi, waliianza Ligi Kuu vema wakionyesha dalili zote za kutetea ubingwa
wao kwa kufanikiwa kuwa kileleni hadi mwishoni mwa mzunguko huo, kabla ya mambo
kugeuka ghafla.
Zilianza
sare kwanza, 1-1 na Yanga, 0-0 na Coastal Union, 2-2 na Kagera Sugar na baadaye
0-0 na Mgambo, 0-0 na Polisi Morogoro kabla ya kufungwa mechi ya kwanza msimu
huu, mbele ya Mtibwa Sugar na kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha 1-0
kutoka kwa Toto Africans.
Matokeo haya
kwa kiasi kikubwa yameivuruga Simba SC na inasemekana Makamu Mwenyekiti wa
klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ anafikiria kujiuzulu na baada ya kufungwa
na Mtibwa Sugar, hakujihusisha na chochote juu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya
Toto, wakati huo Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage yuko bize na shughuli
za kisiasa Dodoma.
Baada ya
mapumziko mafupi, Simba walirudi mazoezini na Desemba wakaenda Zanzibar
kushiriki Kombe la Mapinduzi, ambako walitolewa Nusu Fainali na baada ya hapo,
wakaenda Oman, kwenye kambi ya wiki mbili ya mafunzo. Waliporejea, juzi
walicheza mchezo wa kujipima nguvu na Black Leopard ya Afrika Kusini.
Habari
mbaya, au njema kwa wapenzi wa Simba ni kumpoteza mshambuliaji wake hatari,
Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola za Kimarekani 300,000 katika klabu ya Etoile du
Sahel ya Tunisia. Simba imeingiza fedha nyingi, ambazo ni rekodi katika
historia yao ya kuuza wachezaji, ila wamepoteza kifaa cha maana sana.
Katika
dirisha dogo, Simba imesajili wachezaji wawili tu kutoka Uganda, kipa Abbel
Dhaira na kiungo anayeweza kucheza kama beki pia, Mussa Mudde. Aidha, Simba SC
imebadilisha benchi lake Ufundi, imemuondoa Mserbia, Milovan Cirkovick na
kuleta Mfaransa, Patrick Liewig ambaye atakuwa anasaidiwa na Mganda, Moses
Basena na Mzalendo Jamhiri Kihwelo ‘Julio’.
P W D L GF GA GD Pts
3 Simba SC 13 6 5 2 20 11 9 23
KOCHA: Patrick
Liewig (Ufaransa)
MTIBWA SUGAR:
Ilianza
vizuri, katikati ikavurunda na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza ikazinduka tena
hatimaye imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Inaonekana
Mtibwa Sugar inaanza kurejesha makali yake iliyoingia nayo katika soka ya
Tanzania miaka ya 1990 hadi wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara mbili
mfululizo 1999 na 2000, wakiweka rekodi ya kuwa timu pekee nje ya Simba na
Yanga kutetea taji hilo.
Hiyo si kwa
sababu tu ipo nyuma ya Yanga, Azam na Simba, bali katika mzunguko wa kwanza msimu
huu imefanikiwa kuvifunga vigogo vyote vya soka nchini, Simba na Yanga. Baada ya mapumziko mafupi, Mtibwa walianza
mazoezi Desemba na mapema mwezi huu walikwenda kucheza Kombe la Mapinduzi,
ambako hata hivyo hawakufanya vizuri. Waliporejea Morogoro, waliendelea na
mazoezi na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu. Katika dirisha dogo, Mtibwa
Sugar imesajili wachezaji wane tu, wote huru Rajab Mohamed, Zakayo Joseph,
Baraka Anthony na Mussa Chambo.
P W D L GF GA GD Pts
4 Mtibwa Sugar 13 6 4 3 18 12 6 22
KOCHA: Mecky
Mexime (Mzalendo)
COASTAL UNION:
Wana
Mangushi wamerudi tena kwenye makali yao yaliyowafanya wakawa mabingwa wa ligi
hiyo mwaka 1988, kwani hadi sasa wameonyesha upinzani wa kutosha kwenye Ligi
Kuu. Wagosi hao wa Kaya wamemaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi
Kuu kwa pointi zao 22 sawa na Mtibwa walio nafasi ya nne, lakini wanazidiwa
wastani tu wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo,
Coastal walianza Ligi Kuu kwa kusuasua kiasi cha kufikia kuwafukuza makocha
wake wa awali waliosajili na kuandaa timu kwa ajili ya ligi hiyo, Juma Mgunda
na Habib Kondo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hemed Morcco na Alloy Kiddy.
Baada ya
mapumziko mafupi, Coastal walianza kujifua Desemba na mapema mwezi huu
walikwenda Zanzibar kucheza Kombe la Mapinduzi, ambako hata hivyo hawakufanhya
vizuri. Waliporejea waliweka kambi Tanga wakiendelea kujifua na kucheza mechi
kadhaa za majaribio.
Katika
dirisha dogo, Coastal wamewasajili Shabani Kado kutoka Yanga, aliyekuwa
anacheza kwa mkopo Mtibwa Sugar, Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe
Ramadhan, Castory Mumbara na Tinashe Machemedze, wote huru.
P W D L GF GA GD Pts
5 Coastal Union 13 6 4 3 16 14 2 22
KOCHA: Hemed
Morocco (Zanzibar)
KAGERA SUGAR:
Kagera Sugar
wamemaliza katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 21 na wangeweza kumaliza juu
ya hapo, kama wangeutumia vizuri mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa nyumbani
dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
Wakipewa
nafasi kubwa ya kushinda, katika mastaajabu ya wengi, Kagera wakalazimishwa
sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba,
Bukoba, hivyo kuwapa nafasi Coastal na Mtibwa kuendelea kuwa juu yao.
Kagera inajivunia
kutofungwa na vigogo wa soka nchini, kwani waliifunga Yanga 1-0 na wakatoa sare
ya 2-2 na Simba na Dar es Salaam. Baada
ya mapumziko mafupi, Kagera walianza kujifua Desemba na kupata mechi kadhaa za
kujipima nguvu.
Katika
dirisha dogo, Kagera Sugar wamesajili wachezaji wawili tu na wote huru; Edmund
Kashamila na Julius Mrope.
P W D L GF GA GD Pts
6 Kagera Sugar 13 5 6 2 15 10 5 21
KOCHA:
Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ (Mzalendo)
RUVU SHOOTING:
Katika timu
zote za majeshi kwenye ligi hiyo, Ruvu Shooting ndio inaonekana kuwa imara
zaidi na ndiyo maana ilimaliza katika nafasi nzuri zaidi, ya saba. Ruvu ipo
katikati ya msimamo wa ligi, nafasi ya saba kwa pointi zake 20.
Timu hii
inayotumia Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani ni moja kati ya timu zilizoonyesha
kandanda safi ya kuvutia, tena ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, kama Seif
Abdallah anayegombea kiatu cha dhahabu.
Baada ya
mapumziko mafupi, Ruvu Shooting walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za
kujipima nguvu na katika dirisha dogo, Ruvu Shooting wamesajili wachezaji
watatu tu na wote huru; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu. Habari
mbaya kwa wapenzi wa timu hiyo, ni kumpoteza kinara wake wa mabao katika
mzunguko wa kwanza, Seif Abdallah aliyesajiliwa Azam FC.
P W D L GF GA GD Pts
7 Ruvu Shooting 13 6 2 5 19 17 2 20
KOCHA:
Charles Boniface Mkwasa (Mzalendo)
MGAMBO JKT:
Ligi Kuu ya
Bara imepokea timu mpya tushio ambayo imeongeza ladha katika ligi hiyo. Hiyo si
nyingine zaidi ya JKT Mgambo ua Handeni, Tanga inayotumia Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga pamoja na Coastal Union. Mgambo ilimaliza katika nafasi ya nane, kwa
pointi zake 17. Mgambo walianza kwa kusuasua na watu wakaitabiria itashuka
daraja, ila ilipokuja kuzinduka mwishoni mwa msimu, watu wamebadilisha kauli
zao.
Baada ya
mapumziko mafupi, Mgambo JKT walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za
kujipima nguvu, wakati katika dirisha dogo Mgambo JKT wamesajili wachezaji
watatu, ambao ni Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi.
P W D L GF GA GD Pts
8 Mgambo JKT 13 5 2 6 10 13 -3 17
KOCHA:
Mohamed Kampira (Mzalendo)
JKT RUVU:
Imeshuhudiwa
katika msimu mwingine, timu hii inazidi kupoteza makali yake, baada ya kumaliza
katika nafasi ya tisa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Siyo JKT ile
ambayo ilikuwa tishio kwa vigogo, Simba na Yanga bali hii ya sasa ni ‘urojo’ na
hali hii inatokea huku ikiwa inaundwa karibu na asilimia kubwa ya wachezaji
wake wale wale, walioifanya iwe tishio misimu michache iliyopita, tena wakiwa
chini ya kocha yule yule, kiungo wa zamani wa Yanga, Charles Killinda.
Baada ya
mapumziko mafupi, Ruvu JKT walirudi mazoezini na kupata mechi kadhaa za
kujipima nguvu na katika dirisha dogo, JKT Ruvu imesajili wachezaji wanne,
Zahoro Pazi kwa mkopo kutoka Azam, ambaye hata hivyo amekwenda kufanya
majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini, Emmanuel Linjechele,
Kisimba Luambano na Nashon Naftali.
P W D L GF GA GD Pts
9 JKT Ruvu 13 4 3 6 13 20 -7 15
KOCHA:
Charles Kilinda (Mzalendo)
JKT OLJORO:
Haina makali
yake iliyoingia nayo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita yaliyowafanya wamalize
mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni. Msimu huu JKT Oljoro imemaliza katika
nafasi ya 10 kwa pointi zake 14 na huwezi kusita kusema ipo kwenye hatari ya
kushuka daraja hadi sasa.
Ina pointi
14, sawa na Toto Africans iliyo nafasi ya 11 na inabebwa juu kwa wastani wa bao
moja tu katika mabao ya kufunga na kufungwa, huku ikiwa inaizidi kwa pointi
mbili tu Africans Lyon iliyo nafasi ya 12- JKT Oljoro hakika imemaliza mzunguko
wa kwanza katika eneo baya. Baada ya
mapumziko mafupi, Oljoro ilianza kujifua Desemba mwaka jana na katika kujisuka
upya, ilimfukuza kocha wake Mbwana Makatta, na hadi sasa haijamtaja kocha wake
mpya.
Katika
dirisha dogo, Oljoro imesajili wachezaji wapya wanane, ambao ni Nurdin
Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami
Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter.
P W D L GF GA GD Pts
10 JKT Oljoro 13 3 5 5 13 16 -3 14
KOCHA: Hajatajwa
baada ya Makatta kufukuzwa
TZ PRISONS:
Imerejea
Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa unaweza kusema inapambana kuhakikisha inabaki
kwenye ligi hiyo msimu ujao. Prisons ilimaliza katika nafasi ya 11 ikiwa na
pointi 14.
Ipo katika
hali mbaya na inakabiliwa na vita ngumu ya kupigana kuhakikisha inabaki Ligi
Kuu. Mbaya zaidi katika dirisha dogo, limpoteza beki wake kisiki, David
Mwantika aliyesajiliwa Azam FC.
Hata hivyo,
nayo imejiimarisha katika usajili wa dirisha dogo, baada ya kusajili wapya
wawili, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Gabriel na Mohamed
Kayi, ambao wote ni huru.
Prisons
ilianza kujifua kwa ajili ya mzunguko wa pili tangu Desemba mwaka jana na
imepata mechi kadhaa za kujipima nguvu, hadi za ugenini ikiwemo ya wiki hii
dhidi ya Mtibwa Sugar huko Morogoro, ambako walifungwa 1-0 Manungu.
P W D L GF GA GD Pts
11 TZ Prisons 13 3 5 5 8 12 -4 14
KOCHA:
Jumanne Charles (Mzalendo)
TOTO AFRICANS:
Wana
Kishamapanda bado wapo katika wakati mgumu, kwani walimaliza mzunguko wa kwanza
wa Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ndani ya nafasi tatu za
kushuka Daraja.
Washukuru
sana ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wao wa mwisho wa
mzunguko wa kwanza, kwani umewainua kidogo, vinginevyo wangemaliza ligi hiyo
vibaya zaidi.
Lakini hii
ni timu ambayo inacheza kwa ushindani zaidi inapokutana na timu tishio, ila kwa
timu ambao zinaonekana si tishio, Toto hufanya vibaya. Bila shaka kuna kudharau
mechi, ambako ndiko kunawaponza na kama watabadilika mzunguko wa pili, wanaweza
kufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu. Baada
ya mapumziko mafupi, Toto walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima
nguvu na katika dirisha dogo, waliimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji
wapya wanne, ambao ni Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na
Ulugbe Odia.
P W D L GF GA GD Pts
12 Toto African 13 2 6 5 10 15 -5 12
KOCHA: John
Tegete (Mzalendo)
AFRICAN LYON:
African
Lyon, ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 13 kwa
pointi zalke tisa. Licha ya kunolewa na kocha Muargentina, Pablo Ignacio Velez,
lakini Lyon walikuwa vibonde tu mzunguko wa kwanza.
Mmiliki wa
timu hiyo, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amejitahidi kuboresha kikosi kwa kusajili
wachezaji wapya wa kuongeza nguvu, ingawa si wale alioahidi Emmanuel Okwi na
Mrisho Ngassa wa Simba na Mbuyu Twite wa Yanga.
Katika
dirisha dogo, Zamunda amemudu kuwasajili Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao
wote huru, Ibrahim Job na Shamte Ally wote kwa mkopo kutoka Yanga SC, Buya
Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman,
Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi huru pia.
Aidha,
Mmarekani huyo mwenye asili ya Tanzania, pia amemtupia virago kocha kocha Pablo
Ignacio Velez na kwa sasa timu itakuwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mkenya
Charles Otieno. Lyon imekuwa ikijifua kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe tangu
Desemba mwaka jana, baada ya mapumziko mafupi.
P W D L GF GA GD Pts
13 African Lyon 13 2 3 8 9 20 -11 9
KOCHA: Pablo
Ignacio Velez (Argentina)
POLISI MOROGORO:
Imerejea
Ligi Kuu msimu huu, lakini haitakuwa ajabu mwishoni mwa msimu ikarudi tena
kucheza Ligi Daraja la kwanza. Timu ya Morogoro, ilimaliza mzunguko wa kwanza
wa Ligi Kuu, ikiwa inashika mkia. Polisi haijashinda mechi hata moja zaidi ya
kutoa sare nne na kufungwa mechi nyingine tisa.
Sijui
maajabu gani yatokee, msimu ujao tuendelee kuwa na timu ya Morogoro, kwani
kulingana na ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, hakuna dalili za Polisi kupona.
Lakini hakuna linaloshindikana, timu hiyo inaonekana kufanyia kazi suala hilo
na imeboresha kikosi kwa kusajili wachezaji kadhaa wenye uzoefu wa Ligi Kuu
wainusuru timu, ingawa bahati mbaya kwao, wamepoteza kocha wao John Simkoko.
Katika
dirisha dogo, Polisi Moro imewasajili Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum
Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo
Chomba.
P W D L GF GA GD Pts
14 Polisi Moro 13 0 4 9 4 16 -12 4
KOCHA: adolph
rishard (Mzalendo)
WALIOINGIA
DIRISHA DOGO LIGI KUU BARA:
Yanga SC; Kabange Twite (APR, Rwanda/FC Lupopo DRC)
Coastal FC; Shabani Kado (Kutoka Mtibwa Sugar/Yanga SC)
Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara, Tinashe
Machemedze (Huru).
Azam FC; Humphrey Mieno (Kenya), Brian Umony (Uganda),
Jockins Atudo(Kenya), David Mwantika(Prisons), Abdallah Seif (Ruvu
Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani (mkopo,
Simba SC).
Ruvu Shooting; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na
Mahmoud Mbulu (Huru),
Prisons; Mohamed
Kayi na Emmanuel Gabriel (Huru).
JKT Oljoro; Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa,
Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa
Mbaga na Alphonce Peter (Huru)
Polisi Moro; Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum
Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo
Chomba (Huru)
Kagera Sugar; Edmund Kashamila na Julius Mrope (Huru).
Mtibwa
Sugar; Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo (Huru)
JKT Ruvu; Zahoro Pazi (mkopo, Azam), Emmanuel
Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali (Huru)
Mgambo JKT; Moaka Shabani, Ismail Mkaima na
Damas Milanzi (Huru)
Toto
Africans; Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia (Huru).
African Lyon; Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf
Mgwao (Huru), Ibrahim Job (mkopo, Yanga SC) Shamte Ally(mkopo,
Yanga SC), Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory
Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi (Huru)