Kikosi cha Simba leo. Kiggi wa kwanza kushoto waliosimama |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
KIGGI Makassy
usiku huu amemnusuru kocha Msaidizi wa Simba SC, Jamhuri Mussa Kihwelo kupoteza
ajira yake, baada ya kuifungia timu hiyo bao la kusawazisha dhidi ya Bandari ya
hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar timu
hizo zikitoka sare ya 1-1.
Jamhuri maarufu
kama Julio, aliahidi kujiuzulu na kuogelea kutoka hapa hadi Dar es Salaam, iwapo
Simba ingefungwa na Bandari leo, lakini kwa bao la Kiggi ailyechezeshwa beki ya
kushoto leo, amenusurika na adhabu hiyo.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia
kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi
Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa
penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la
hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na
mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi
alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita
20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.
Kipindi cha
pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo,
Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude,
Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao
Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo
hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano
hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama
mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Kikosi cha Simba
SC leo kilikuwa; Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Kiggi Makassy, Hassan Hatibu,
Shomary Kapombe, Mussa Mude/Haruna Chanongo dk46, Ramadhan Singano ‘Messi’/Jonas
Mkude dk46, Abdallah Seseme, Christopher Edward, Salim Kinje/Mwinyi Kazimoto
dk46 na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Bandari FC; Hassan
Hajji/Ahmad Suleiman dk48, Saleh Nassor, Othman Juma, Haitham Juma, Kassim
Hariri, Rashid Omary, Sharrif Kitwana, Mohamed Nassor, Mussa Omary, Amour Janja
na Fauzi Ally.