Chanongo akimshukuru Kiggi kwa kona ya bao |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
KIUNGO wa
Simba, Kiggi Makassy jana alimpamia kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo
katika mazoezi kwenye Uwanja wa Fuoni, visiwani hapa wakati anawahi mpira
akapige kona na hilo limehusishwa na kutolewa kwake dakika ya 27 katika mechi
ya juzi, lakini uongozi wa klabu hiyo umesema hakuna kitu kama hicho.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Ufundi ya Simba SC, Daniel Manembe amesema hakuna ugomvi kati ya
Kiggi na Julio, bali kama ilivyo kawaida ya wanadamu, baada ya tukio hilo la
jana maneno yameanza kuwa mengi.
“Ilikuwa
bahati mbaya, yule anawahi mpira akapige kona, akampamia Julio kwa bahati
mbaya, naomba tafadhali msilitafsiri vibaya tukio hilo, hakuna tofauti yoyote
kati ya Julio na Kiggi,”alisema Manembe.
BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo imeripoti kuwa Makassy
hafurahii maisha Simba SC na lolote linaweza kutokea juu yake wakati wowote.
Kiungo huyo
aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu kutoka mahasimu Yanga, amekutana na kile
amabcho alikimbia timu yake ya zamani, benchi mfululizo.
Katika
mchezo wa juzi wa Kombe la Mapinduzi visiwani hapa, Kiggi alionyesha dhahiri
kuchukizwa na kitendo cha kutolewa dakika ya 27 nafasi yake ikichukuliwa na
Edward Christopher.
Akitoka
kupiga maridadi iliyounganishwa nyavuni na Haruna Chanongo, Kiggi aliitwa
benchi kumpisha Edward na alionekana kutoka kwa huzuni na alipofika benchi
alikataa hata kupokea chupa ya maji aliyopewa.
Habari zaidi
zinasema, tayari Kiggi amekwishaanza mishemishe za kusaka timu nyingine ya
kwenda kuchezea baada ya kuona yupo katika wakati mgumu Simba SC.
Simba SC leo
inashuka tena dimbani kumenyana Tusker ya Kenya katika mchezo wa pili wa Kundi
A, baada ya kushinda 4-2 dhidi ya Jamhuri ya Pemba juzi. Je, Kiggi atapangwa?
Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.