KAMPUNI tano
zimewasilisha tenda zao kuomba kupewa kazi ya kukarabati hosteli ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Januari 7 mwaka huu TFF ilitangaza tenda kwa
ajili ya ukarabati wa hosteli hiyo baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) kukubali ombi lake la kutoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Ufunguzi wa
tenda hizo ulifanyika jana (Januari 28 mwaka huu) kupitia kwa Bodi ya Tenda ya
TFF mbele ya wazabuni wote watano waliowasilisha tenda zao na kushuhudiwa pia
na Mkandarasi mshauri. Wazabuni (kampuni) waliojitokeza awali walikuwa saba,
lakini waliorejesha zabuni zao ni watano.
Kampuni hizo
ni Crescent Concrete Limited, DGS Company Limited, Mart Builders Company
Limited, Prince General Investment Limited na Send Star Company Limited.
Bodi ya
Tenda ya TFF itakutana Januari 31 mwaka huu pamoja na mambo mengine kuchagua
kampuni ambayo itafanya ukarabati huo.