Liewig akiwa na wasaidizi wake katika mchezo wa jana wakijadiliana kabla ya mechi |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
KOCHA Mkuu
wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig amekubali yote kutokana na mechi ya timu yake
jana dhidi ya Tusker ya Kenya, lakini amekerwa na jambo moja tu, timu yake
kutaka kufunga mabao mepesi.
Akizungumza na
BIN
ZUBEIRY baada ya mechi ya jana, Liewig alisema timu inabadilika
taratibu na anaamini watafanikiwa kuwa na timu bora, lakini jambo moja tu
amesema wachezaji wake lazima wabadilike haraka wanapofika kwenye eneo la
hatari la wapinzani kwa kuonyesha uchu.
“Wanapofika
kwenye eneo la hatari la wapinzani, wanakuwa wanataka kufunga bao la rahisi
sana, hapana, wakati mwingine lazima ujifunze kufunga bao katika mazingira magumu.
Hili lazima tulifanyie kazi haraka na wachezaji wabadilike,”alisema Liewig.
Simba SC jana
ilitoka sare ya kufunga bao 1-1 na
Tusker ya Kenya katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa
Amaan mjini hapa.
Kwa matokeo
hayo, Tusker inaendelea kuongoza Kundi A, kwa piointi zake tatu sawa na Simba,
lakini mabingwa hao wa Kenya wana wastani mzuri zaidi wa mabao.
Hadi
mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba wakitangulia
kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi Shaaban, maarufu kama Boban au
Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha dakika ya 39, mfungaji Khalid
Aucho.
Boban
alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu akiwa amedhibitiwa na beki
ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia pasi ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’
kuitumbukiza nyavuni.
Baada ya
kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono na kuumia, hivyo hakushangilia bao
lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
Baada ya bao
hilo, Simba iliongeza mashambulizi langoni mwa Tusker na Boban alikaribia
kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache.
Aucho
alifunga bao lake akiunganisha krosi ya Jeremiah Bright kutoka upande wa
kushoto wa Uwanja.
Baada ya
hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza
kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
Kipindi cha
pili timu zote zilirudi vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo
ambalo lilisababisha dakika 90 zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema,
Shomary Kapombe, Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani/MKussa Mudde75, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’/Edward
Christopher dk 52.
Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke Ochieng,
Jeremiah Bright/Humphrey Okoth, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho,
Edwin Manono/Benson Amanda, Justin Monda, Ismail Dunga/Michael Olunga, Jesse
Were na Robert Omonuk.
Katika
mchezo uliotangulia, Jamhuri ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Bandari kwenye Uwanja
wa Mao Dze Tung. Mabao ya Jamhuri yalifungwa na Fahad Abdallah Athumani dakika
ya 25 na Ally Bilal dakika ya 67, wakati la Bandari lilifungwa na Faudhi Ally
dakika ya tano.