Abdulfatah akiwa Nahodha wa Simba SC, Juma Kaseja |
Abdulfatah Salim Saleh |
Na Mahmoud Zubeiry
HIVI karibuni, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage
alitaja Kamati mpya ndogo ndogo za klabu hiyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hiyo ilifuatia baadhi ya Wajumbe kutotekeleza majukumu yao vizuri,
hali ambayo ilisababisha klabu hiyo kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya
Bara ikiwa katika nafasi ya tatu, na hivyo kuweka rehani taji lake la ubingwa
wa ligi hiyo.
Simba ilimaliza na pointi 24 mzunguko huo, ikiwa inazidiwa
pointi tano na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC waliomaliza kileleni na kuzidiwa
pia pointi moja na Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili na pointi 25.
Miongoni mwa watu wapya katika Kamati za Simba SC, ni milionea
kijana mwenye umri wa miaka 32, Abdulfatah Salim Saleh, ambaye yeye ni Mjumbe
wa Kamati ya Mashindano.
Abdulfatah |
Abdulfatah ni nani?
Ni mfanyabiashara na mmiliki wa hoteli maarufu Dar es Salaam,
ambazo ni Sapphire iliyopo Kariakoo, Mtaa wa Sikukuu na Lindi na Al Uruba iliyopo
Mtaa wa Mkunguni na Sikukuu, Kariakoo pamoja na maduka ya jumla ya vifaa vya
mbalimbali, yaitwayo Al Ahly Diaper’s yaliyopo Mtaa wa Aggrey na Nyamwezi, na lingine
Mtaa wa India na Moscow na nyumba za kupangisha (apartments) ziitwazo Samsa
Real Estate Limited, zilizopo barabara ya Morocco.
Ni kijana anayeendeleza utajiri wa ukoo wao, mfano wa
wafanyabiashara wengine vijana waliondeleza vema bishara za wazazi wao, kama
Yussuf Manji, Mohamed Dewji, Abubakar Bakhresa na wadogo zake, Abdallah Bin
Kleb na wengineo.
Abdulfatah |
Abdelfatah na Simba SC
Abdulfatah alianza kuipenda Simba tangu akiwa mdogo, anasoma
shule ya Msingi St. Austine Academy Nairobi, Kenya na kila alipokuwa likizo Dar
es Salaam alikuwa hakosi mechi za timu hiyo.
Anasema kilichomshawishi kuipenda Simba SC ni baba yake mdogo,
Hassan Afif aliyeichezea na kuifundisha klabu ya Simba miaka ya 1990 mwanzoni. “Wakati
baba mdogo anakuwa kocha mchezaji na kuipa Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na
Kati mwaka 1991, nilihudhuria mechi zote hadi wanachukua ubingwa kwa kuifunga
SC Villa ya Uganda, wakati huo nilikuwa likizo hapa,”anasema.
Abdullfatah anasema wakati huo pia alikuwa anacheza mpira katika
nafasi ya mshambuliaji na alikuwa ana ndoto za kufuata nyayo za baba yake mdogo
kuvaa uzi wa Simba, lakini baba yake mzazi alimkataza na kutaka atilie mkazo
masomo.
“Baba alitaka nisome tu ili nije kuendeleza biashara, lakini
ukiuliza niliocheza hata hapa Dar es Salaam wakati wa utoto, watakuambia
nilikuwa mshambuliaji hatari sana,”anasema.
Abdulfatah akiwa na mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi ambaye ameuzwa Etoile du Sahel ya Tunisia |
Ameingizwaje Kamati ya Mashindano?
Anasema kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara na ni mwanachama wa Simba
SC, aliamua kuisaidia klabu yake sehemu ya kuwekea kambi kwa gharama nafuu na
kusaidia baadhi ya mambo, ambayo hakupenda kuyataja.
Kutokana na hilo, Abdulfatah anasema alijikuta anakuwa karibu
na viongozi wa Simba SC, ambao aliiva nao kiasi cha kuamua kumuingiza kwenye Kamati
hiyo.
Anasema kwa moyo mkunjufu amekubali majukumu hayo na
atashirikiana na wajumbe wenzake pamoja na Kamati ya Utendaji, kuhakikisha
Simba SC inafanya vizuri katika mashindano yoyote inayoshiriki.
“Tunaanza Ligi Kuu kesho, timu imetoka Oman, imefikia katika
kambi nzuri kwenye hoteli yangu hapa Sapphire, wachezaji wanaishi vizuri na wanafurahi
na wana ari kubwa, kuna matumaini ya ushindi, na tutahakikisha ubingwa wa Bara
tunachukua na kwenye Ligi ya Mabingwa tunafika mbali”anasema.
Huyo ndiye Abdulfatah, baba wa watoto watatu, milionea kijana
anayeipiga jeki Simba SC.