Dhaira akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kushoto |
Na Prince Akbar
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira sasa anatarajiwa kuwasili leo saa 8:00 mchana
kujiunga na klabu yake mpya, Simba SC ya Dar es Salaam, baada ya kushindwa
kutokea jana.
Dhaira
aliyesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Kimarekani 40,000,
na mshahara wa Sh. Mlioni 2 kwa mwezi, awali alitarajiwa kuwasili jana, lakini
akaahirisha safari na sasa anatarajiwa leo.
Uongozi wa
Simba umesema Dhaira akifika Dar es Salaam ataunganishiwa usafiri wa kwenda
moja kwa moja Zanzibar, ambako Simba inashiriki Kombe la Mapinduzi.
Dhaira aliyeibukia
Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo
aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisoteshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja ameendelea kuitwa kwenye kikosi cha timu ya
taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa
ukweli.