Felix Sunzu kushoto akitibiwa na Dk Cossmas Kapinga wa Simba kulia katika moja ya mechi za Ligi Kuu mzunguko wa kwanza msimu huu |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA wa Simba SC, Abbel Dhaira na beki Mussa Mude wote raia
wa Uganda waliokuwa majeruhi wamepona na leo wamefanya mazoezi na timu yao kwenye
Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Hata hivyo, wachezaji wengine wa timu hiyo wanne leo
wameshindwa kufanya mazoezi kwa sababu mbalimbali.
Msemaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wachezaji ambao
hawajafanya mazoezi leo ni beki Paul Ngalema, viungo Jonas Mkude, Ramadhani
Singano ‘Messi’ na mshambuliaji Felix Sunzu, raia wa Zambia.
“Hawa wana kesi tofauti, wengine Malaria wengine maumivu
maumivu tu madogo, lakini kuna matumaini kesho wataendelea na mazoezi,”alisema
Kamwaga.
Lakini kurejea kwa Dhaira ni faraja kwa wapenzi wa timu hiyo,
wenye hamu ya kumuona kwa mara ya kwanza akiwa amesimama kwenye milingoti
mitatu tangu asajiliwe kutoka Uganda.
Kipa huyo namba moja wa Uganda, hakuingizwa kwenye programu
ya mechi ya kwanza ya timu yake ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara juzi dhidi ya African Lyon kutokana na maumivu ya nyonga.
Katika mchezo huo, ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao
3-1, ‘Tanzania One’ Juma Kaseja alianza langoni na kufanya kazi nzuri, ikiwemo
kuokoa mkwaju wa penalti ya Shamte Ally.
Hata hivyo, refa Israel Mujuni aliyetoa penalti hiyo
baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua Fred Lewis, aliamuru irudiwe kwa madai
Kaseja alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje
kabisa.
Kwa upande wake, Mudde kiungo Mganda ambaye sasa anarudishwa
kucheza nafasi ya ulinzi, Mussa Mudde alitolewa kipindi cha pili kwenye mechi
dhidi ya Lyon, kutokana na kuumia misuli, lakini naye yuko fiti na ameanza
mazoezi tena.
Aidha, Kamgwa alisema kikosi cha Simba SC kinarudi kambini
leo, katika hoteli maridadi na adilifu ya Sapphire, iliyopo Kariakoo, Dar es
Salaam, kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu, dhidi ya JKT Ruvu, Februari 3,
mwaka huu.